Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) kwa kushirikiana na Jumuiya ya Ulaya (EU) inaendesha warsha ya kuboresha shughuli za kisheria na uhakiki ili kuboresha uwezo uliopo katika kudhibiti madini ya urani.
Warsha hii ya siku tatu ambayo imeanza tarehe 19 hadi tarehe 21, Novemba 2019 katika makao makuu ya TAEC yaliyopo Njiro, Arusha.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania(TAEC),Pro.Lazaro Busagala (aliyekaa katikati) katika picha ya pamoja na washiriki wa warsha ya majadiliano ya pamoja ya sheria ya udhibiti wa uchimbaji salama wa madini ya Urani.
Lengo la warsha hii ni kujadili tathimini ya ripoti ya Sheria ya udhibiti na mahitaji na ya leseni ya uchimbaji wa madini ya urani. Pia katika warsha hii muhitasari wa uwepo wa madini ya urani pamoja na utayari wa utoaji wa leseni ya uchimbaji wa madini ya urani katika siku zijazo pia utajadiliwa.
Mkurugenzi Mkuu wa TAEC, Profesa Lazaro Busagala akifungua warsha hiyo kwa niaba ya Mhe. Naibu Waziri wa Wizara ya Madini, amesema majadiliano ya warsha yanalenga kuja na sheria mpya itakayoweza kutumika katika uchimbaji wa madini ya Urani pamoja na kumlinda mwananchi wa kawaida na madhara ya madini hayo.
“Kunahitajika udhibiti wa hali ya juu katika madini ya urani, hivyo sheria mpya itakapokamilika itaanza kutumika “alisema Prof.Lazaro .
Jumla ya washiriki 29 wanashiriki katika warsha hii ambapo washiriki ishirini (20) ni kutoka TAEC na washiriki wengine tisa (9) ni kutoka taasisi nyingine ambazo zinahusika katika maswala ya madini ya urani kama vile, Wizara ya Madini, Wizara ya elimu, Sayansi na Teknolojia, Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Wizara ya Maji, Wizara ya Maliasili, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu na Tume ya Madini.