Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Walemavu, Mhe Stella Ikupa akikata utepe kuashiria kufungua Soko la Buigiri ambapo litatumika na watu wenye ulemavu waliomaliza mafunzo ya Ujasiriamali.
Mkurugenzi wa Taasisi ya NAKUA NA TAIFA LANGU, Jessica Mshama akizungumza na wahitimu wa mafunzo hayo ambayo Taasisi yake imekua ikiendesha. Kushoto ni Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Stella Ikupa.
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Walemavu, Mhe Stella Ikupa akisikiliza maelezo ya mmoja wa wahitimu wa mafunzo ya Ujasiriamali katika Kata ya Buigiri wilayani Chamwino ambalo baadhi ya bidhaa wanazozitengeneza ni pamoja na Siagi ya Karanga na Ubuyu.
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Stella Ikupa akizungumza na wahitimu wa mafunzo ya Ujasiriamali wilayani Chamwino, Dodoma.
Diwani wa Kata ya Buigiri, Kenneth Yindi akizungumza na wahitimu wa mafunzo hayo ya Ujasiriamali wapatao 200 ambao ni Walemavu na Wanawake.
Naibu Waziri Stella Ikupa akimkabidhi cheti cha kuhitimu mafunzo ya Ujasiriamali yaliyotolewa na Taasisi ya NAKUA NA TAIFA LANGU katika Kata ya Buigiri Wilayani Chamwino.

Na Charles James - Dodoma.

SERIKALI imesema itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kutoa elimu kwa watu wenye uhitaji maalum ili kuweza kuwanasua katika kundi la ombaomba na kuwafanya wawe tegemezi kwa kuwa na miradi yenye kuwapa kipato.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia watu wenye ulemavu, Mhe Stella Ikupa wakati alipokua akifunga mafunzo ya Ujasiriamali kwa watu wenye ulemavu katika Kata ya Buigiri Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma.

Mafunzo hayo yalianza toka Novemba 29 ambapo yaliandaliwa na Taasisi ya NAKUA NA TAIFA LANGU kwa kushirikiana na Diwani wa Kata hiyo Mhe Kenneth Lindi ambapo yalihusisha watu wenye ulemavu na wanawake.

Elimu iliyotolewa ni Elimu ya kujitambua, Elimu ya usindikaji bidhaa kwa vitendo, Elimu ya masoko, Athari ya matumizi ya rushwa katika upatikanaji wa huduma, Umuhimu na utaratibu wa kuunda vikundi vya walemavu na wanawake pamoja na Elimu ya matumizi sahihi ya fedha za mikopo.

Akizungumza na wahitimu hao, Naibu Waziri Ikupa amempongeza Mkurugenzi wa Taasisi hiyo ya NAKUA NA TAIFA LANGU, Jessica Mshama kwa uzalendo aliouonesha kwa kuamua kutoa elimu kwa watanzania wenzake ambayo itawaondoa kwenye lindi la umaskini.

"Nikupongeze sana Jessica umefanya jambo kubwa siyo tu kwa Wananchi wa Buigiri bali kwa Taifa lako kwa ujumla. Elimu hii uliyowapa ina manufaa makubwa kwao wenyewe na hata kwa kizazi chao. Niwaahidi Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wote wa maendeleo katika kuwakomboa watu wetu," Amesema Mhe Ikupa.

Amesema ili kufikia uchumi wa kati kupitia viwanda ni lazima kila kundi nchini lihusike katika uzalishaji na kuwapongeza wahitimu hao kwa kuelewa mafunzo vizuri na kuanza kutengeneza bidhaa zao ikiwemo Ubuyu, Siagi ya Karanga pamoja na Sabuni.

Nae Mkurugenzi wa NAKUA NA TAIFA LANGU, Jessica Mshama amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwapa elimu ya kujitegemea watu wenye ulemavu ili kuepukana na dhana ya kwamba walemavu wote ni ombaomba.

Amesema Serikali ya awamu ya tano imepiga hatua kwenye maendeleo hivyo wao kama wadau wana kila sababu ya kusaidia Rais Magufuli katika kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

"Mhe Waziri tunashukuru kwa kufungua na kufunga mafunzo haya. Tunakuahidi kuwa Taasisi yetu itaendelea kutoa mafunzo haya Nchi nzima lakini pia kuwatafutia masoko ya bidhaa wanazotengeneza hawa wahitimu.

Tayari Dodoma tushatoa elimu kwa watu 300 hapa Chamwino na Wilaya ya Chemba, tutaenda Kongwa, Mpwapwa na Wilaya zingine. Lakini lengo letu ni kuona tunawainua kiuchumi walemavu na wanawake nchini," Amesema Jessica.

Kwa upande wake Diwani wa Kata hiyo, Kenneth Yindi ameishukuru Serikali na Taasisi hiyo kwa kutoa mafunzo hayo ambayo anaamini yataenda kubadilisha mtazamo na fikra za wananchi wa Kata ya Buigiri.

Amesema mafunzo hayo yamewasaidia kuweza kujitambua na kutengeneza bidhaa mbalimbali ambazo zitakua na nembo ya Buigiri jambo ambalo litasaidia Kata yao kukua kimaendeleo na kuvutia watu kuja kuwekeza na hivyo kuongeza mapato ndani ya Halmashauri yao.

"Hakika tunaipongeza Taasisi ya NAKUA NA TAIFA LANGU kwa kuendesha mafunzo haya, wametoa kiasi cha Sh Milioni Tatu za ueneshaji sambamba na walimu wawili, huu ni uzalendo mkubwa waliouonesha kwetu na tuwaombe waendelee kushirikiana na Serikali yetu ili kufikia kundi kubwa la watu wenye uhitaji," Amesema Yindi.

Mmoja wa wahitimu wa mafunzo hayo, John Masaka ameishukuru Serikali kwa kuendelea kushirikiana na wadau wa Maendeleo katika kufanikisha inawakomboa wananchi wake na kuahidi kutumia mafunzo hayo vizuri ili kujipatia kipato na kuepukana na dhana ya kwamba watu wa Dodoma ni ombaomba.

Pamoja na kuwakabidhi vyeti vya kuhitimu Naibu Waziri Ikupa alifungua pia Soko la Buigiri kwa ajili ya walemavu hao na kumtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Chamwino kuwaongezea kiasi cha Sh Milioni Tatu ili waweze kukuza mitaji yao.