Waasi katika jimbo la Ituri wamekishambulia kituo cha Ebola kinachomilikiwa na shirika la afya duniani WHO, katika uvamizi uliofanyika usiku wa kuamkia Alhamisi na kuwauwa wahudumu watatu.

Taarifa zinasema kuwa miongoni mwa watu waliouawa ni wafanyakazi wa Wafanyakazi wa shirika la afya duniani na kwamba watu wengine wanne wamejeruhiwa vibaya.

Magari manne pia yamechomwa moto pamoja na nyumba kadhaa za kituo hicho pia zimeteketea baada ya polisi wacache wa ulinzi waliokuwa kwenye kituo hicho kushindwa kudhibiti mashambulio hayo ya waasi.

Shambulio hili limelaaniwa na Shirika la Afya Duniani(WHO). Kupitia ujumbe wake wa Twitter , maafisa wakuu wa shirika hilo akiwemo Mkurugenzi Mkuu Bwana Tedros Adhanom Ghebreyesus wamelaani shambulio hilo kwenye kituo cha Ebola lililosababisha vifo na majeruhi:

Mashambulio ya Wanamgambo na ukosefu wa imani ya jamii kwa wafanyakazi wa afya mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Kongo yamekuwa ni kikwazo cha juhudi za kudhibiti mlipuko wa hivi wa Ebola ambao ni hatari kwa taifa gilo na mataifa mengine jirani.

Si mara ya kwanza kwa mashambulio ya aina hii kutokea dhidi ya vituo vya matibabu ya Ebola.

Makundi ya waasi yenye silaha yamekuwa yakishambulia mara kwa mara vituo vya tiba ya Ebola, huku kukiwa kuna ukosefu wa imani miongoni mwa jamii za wakazi wa maeneo yaliyoathiriwa na Ebola ambao walaumu wageni kwa mlipuko ni masuala yanayofanya juhudi za kukabiliana na mlipuko huo kuwa ngumu katika majimbo yenye mizozo ya Ituri na Kivu.