” Alipoletwa nilichuma fimbo katika mti wa mparachichi na kumchapa kwa nia ya kumkanya kama mzazi, wakati namchapa Naomi akasema amechoka, mi nilizani ni utani kwasababu ya kukimbia na ujeuri wake, nilimnyanyua na kumweka barazani, nikaenda kutafuta dawa, nilivyorudi nilikuta amelegea sana, nikachukua gari ya jirani na kumpeleka hospitali Temeke amapo daktari alitufahamisha kuwa Naomi alifariki dunia” Hivyo ndivyo Esther Lyimo (47) alivyo jitetea baada ya kukutwa na hatia ya mauaji ya mjukuu wake.

Aliendelea kusimulia kisa hicho “Mnamo Machi 25, mwaka 2016 wakati natoka kufanya usafi Saloon kwangu, nilielezwa na Andrew kuwa Naomi ameamka, amejikojolea yupo barazani.”

“Nilipoingia ndani nlimwambia Naomi akapige mswaki, lakini aliendelea kukaa barazani , Andrew akaniambia tena hapigi mswaki anachezea maji, nikaongea kwa sauti kwamba nikitoka ndani nitamchapa, nilipotoka Naomi akakimbia nikamwambia Andrew amkamate”.

Ester amesema alikuwa anakaa na watoto wa dada yake na aliwachukua baada ya kuombwa awasomeshe kwa kuwa dada yake hakuwa na uwezo ambapo aliishi nao nyumbani kwake Tuangoma Kigamboni kwa takribani miezi kumi japo walikuwa watundu.

“Watoto hao ni watundu sana, huwa wanakimbizana na kucheza vichakani ambako huku nako kuna mapori kama kilimanjaro hivyo ndio maana mwili wake ulikuwa na vidonda na makovu, sijamuua Naomi, nilikuwa nawapenda”.

Hapo jana, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imemuhukumu kunyongwa hadi kufa mwanamke Esther Lyimo (47) baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mjukuu wake Naomi John (7) kwa kipigo.

Hukumu hiyo imesomwa Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Pamela Mazengo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliyopewa mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa na mashahidi tisa wa upande wa mashitaka na utetezi.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mazengo amesema upande wa mashtaka umeweza kuthibitisha pasipo kuacha shaka kuwa kifo cha naomi kimetokana na kipigo na majeraha ya bibi yake hivyo ametiwa hatiani kwa kosa la kumuua kwa kukusudia Naomi John.

Hakimu Mazengo amesema “adhabu katika kosa la mauaji ni moja tu ni kunyongwa hadi kufa,” hivyo mahakama inakuhukumu kunyongwa hadi kufa”

Lakini Ester aliiomba mahakama impunguzie adhabu kwa sababu hilo ni kosa lake la kwanza pia ana familia inayomtegemea na amekaa gerezani miaka 3.

Hata hivyo imeelezwa kuwa Kulingana na ripoti ya daktari iliyoonesha marehemu alikutwa na majeraha mwilini huku mshtakiwa mwenyewe alikiri kiwa alimchapa marehemu kwa fimbo ya mpera, hiyo inaonesha wazi kuwa aliua kwa kukusudia.

Moja ya ushahidi wa upande wa mashtaka ulidai kuwa, mshtakiwa alimpiga marehemu, kumng’ata mwilini na kisha kumwagia maji ya moto ya chai ambapo inadaiwa ilikuwa tabia yake kuwafanyia ukatili watoto hao Andrew na marehemu Naomi.