Mwanasiasa wa upinzani nchini na aliyekuwa mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA), Tundu Lissu amesema atarejea Tanzania baada ya marafiki zake kumhakikishia usalama wake.
Ametoa kauli hiyo jana akihojiano na kituo cha televisheni cha KTN cha nchini Kenya baada ya kuulizwa kuhusu mpango wake wa kurejea nchini.
“Hali ya usalama wangu bado si nzuri, nafikiri hakuna mtu anayetaka kuona narudi nyumbani kesho na keshokutwa ninapigwa risasi tena. Bado kuna vitisho vya aina hii, watu wenye busara lazima wakae na kuangalia namna nzuri ya kufanya ili niweze kurudi nyumbani kuendelea na shughuli zangu lakini nikiwa salama.” asema.
“Hizi jitihada zinafanywa na marafiki wa ndani na nje ya nchi kuhakikisha nakuwa salama kurudi Tanzania. Ikifika mahala wakasema usalama wangu utaangaliwa nitarudi nyumbani.” ameeleza.
Mwanasheria mkuu huyo wa CHADEMA kwa sasa Lissu yupo Nairobi nchini Kenya.
Ikumbukwe Septemba 7, 2017, Lissu alishambuliwa kwa risasi akiwa kwenye gari nje ya makazi yake Area D jijini Dodoma akitoka kuhudhuria vikao vya Bunge.