Wakati mjadala ukiibuka ndani ya jamii kuhusu uwezekano wa watuhumiwa wa madawa ya kulevya kupatiwa msamaha au la pindi wanapokiri makosa yao, imebainika kuwa uwezekano huo upo kwa mujibu wa sheria, Gazeti la Ijumaa limechambua.
Mjadala huo uliibuka baada ya Mfanyabiashara, Abdul Nsembo maarufu Abdulkandida (45) kuandika barua ya kukiri kosa lake na kuomba msamaha kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Tanzania (DPP).
Nsembo na mkewe, Shamim Mwasha (41), wanakabiliwa na shtaka moja la kusafirisha madawa ya kulevya ‘unga’ aina ya heroin, kinyume cha sheria, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar.
Hata hivyo, Novemba 11, mwaka huu, Nsembo kupitia wakili wake, Benedict Ishabakaki, aliieleza mahakama hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Kelvin Mhina kuwa, mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo (Abdul Nsembo) amemuandikia DPP (Mwendesha Mashtaka) barua ya kuomba msamaha na kukiri shtaka lake, hivyo anasubiri majibu.
DPP AFUNGUKA
Gazeti la Ijumaa lilizungumza na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), Biswalo Mganga ambaye alimtaka mwandishi kuutumia ufafanuzi uliomo katika Sheria ya Makosa ya Jinai kifungu cha 194 ambacho kipengele cha makubaliano ya kukiri kosa (Plea Bargaining) kimefafanua zaidi.
WANASHERIA WAFUNGUKA
Hata hivyo, Gazeti la Ijumaa lilizungumza na Mratibu wa Mtandao wa Utetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo Olengurumwa kupata ufafanuzi ambaye pamoja na mambo mengine, alikiri kuwa upo uwezekano kwa mujibu wa taratibu.
Olengurumwa alisema kwa mujibu wa sheria hiyo ya makosa ya jinai, kifungu cha 194 (F) imebainisha wazi kuwa mtuhumiwa yeyote wa madawa ya kulevya anaweza kupatiwa msamaha baada ya kukiri kosa lake iwapo atakuwa amekamatwa na mzigo wa madawa ya kulevya usiozidi thamani ya shilingi milioni 10. “Ukizidi milioni 10, hapewi msamaha, sasa hapo inategemea hao akina Shamim kwa mfano walikamatwa na mzigo wa thamani gani,” alisema.
Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Anna Henga alianza kufafanua maana ‘Plea Bargaining’ kuwa ni makubaliano maalum katika kesi ya jinai kati ya Mwendesha Mashtaka na mshitakiwa ambapo mshitakiwa anakubali kukiri kosa moja au zadi katika makosa aliyoshitakiwa nayo ili apate nafuu ya kesi hiyo.
Licha ya kuunga mkono hoja ya Olengurumwa, Henga kwa mujibu wa Sheria ya Makosa ya Jinai sura namba 20, iliyofanyiwa marekebisho kupitia Muswada namba 4 wa mwaka 2019 imetoa nafasi kwa watuhumiwa hao kupatiwa msamaha. Alisema makubaliano hayo ya kukiri kosa yameanzia kifungu cha 3 na kuongeza kifungu cha 194A hadi 194H cha Sheria ya Makosa ya Jinai ya Mwaka 1985 (Sura ya 20).
MAKOSA YASIYORUHUSIWA KUFANYIWA MAKUBALIANO
Henga aliyataja makosa hayo kuwa ni ya udhalilishaji wa kingono yenye adhabu ya kufungwa zaidi ya miaka mitano au udhalilishaji dhidi ya mtu aliye chini ya umri wa miaka 18. “Makosa ya uhaini, makosa ya kumiliki au kusafirisha madawa ya kulevya yenye thamani inayozidi shilingi milioni 10 na ugaidi.
“Makosa ya kumiliki nyaraka za Serikali zenye thamani inayozidi shilingi milioni 10 bila idhini ya Mkurugenzi wa Mashtaka na makosa mengine yoyote yatakayoelekezwa na waziri husika,” alisema. Aidha, aliongeza kuwa matokeo ya Makubaliano Maalum ya Kukiri Kosa (Plea Bargaining) ni kwamba Mwendesha Mashtaka anaweza kupunguza makosa makubwa katika hati ya mashtaka na kuacha makosa madogo au kufuta kabisa makosa mengine.
“Mshtakiwa anaweza kukiri kosa aliloshtakiwa kwa makubaliano ya kufutwa kwa makosa mengine. “Pia mshtakiwa anaweza kuamriwa kurudisha au kulipa fidia ya vitu vilivyopatikana kwa njia ya uhalifu au vilivyotumika wakati wa kutenda uhalifu,” alisema.
KESI YENYEWE
Washtakiwa Abdul Nsembo na mkewe, Shamim Mwasha walirudishwa rumande kutokana na shtaka la kusafirisha madawa ya kulevya kutokuwa na dhamana kwa mujibu wa sheria.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, washtakiwa hao wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 36/2019. Kwa pamoja, wanadaiwa kusafirisha madawa ya kulevya aina ya heroin yenye uzito wa gram 232.70, wakati wakijua kufanya hivyo ni kosa kisheria. Wanadaiwa kutenda kosa hilo, Mei mosi, 2019 katika eneo la Mbezi-Beach jijini Dar.
MSAMAHA WA JPM
Hadi Oktoba 12, mwaka huu, jumla ya watuhumiwa 700 wa kesi za uhujumu uchumi kote nchini, walikuwa wamekwishawasilisha barua za maombi kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kwa nia ya kukiri makosa na kuomba msamaha.
Rais Dk John Magufuli alipokuwa Katavi mkoani Rukwa alisema kati ya hao 700 tayari 138 wamepewa msamaha na wameachiwa huru na wako na familia zao huku tayari sehemu ya fedha wameanza kulipa.
“Wale wengine 500 na kitu ambao ‘documents’ zao zinaendelea kuchambuliwa, nao wataachiwa hivyohivyo kadiri watakavyokuwa wanarudisha hizo fedha na hizo fedha zitaendelea kutumika kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania wakiwemo wana- Katavi,” alisema Rais Magufuli na kuongeza;
“Na huu ni upendo wa pekee kwa sababu tulitoa msamaha na wao wameupokea msamaha na sisi tunamshukuru Mwenyezi Mungu aliyewagusa wao na kutubu makosa yao na kuomba msamaha, hao sasa ni raia wema na wahesabike kama raia wema katika nchi yetu.