

SERIKALI imesema imeokoa wastani wa Sh.bilioni 34 katika miaka mitano ya kwanza kutokana na kutumia mfumo wa ununuzi kwa njia ya kieletroniki.
Akizungumza na waandishi habari jijini Dar es Salaam leo Novemba 11,2019, Katibu Mkuu na Mlipaji Mkuu wa Serikali Doto James amesema kwa kuzingatia mfumo huo imeiagiza Mamlaka ya Kudhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA) kuhakikisha ifikapo Desemba 31 mwaka huu kuwa taasisi zote za ununuzi nchini ziwe zimeungwa katika mfumo wa ununuzi kwa njia ya kieletroniki na kuanza kuutumia bila kisingizio chochote.
Katibu Mkuu James amesema kuwa kuzingatia kwa fedha zitumikazo katika utekelezwaji wa miradi ya Serikali kwa kiasi kikubwa hutumika kupitia mifumo ya ununuzi wa umma na kwamba jitihada mbalimbali zimekuwa zikifanyika kuliimarisha eneo hilo ili kuiwezesha Serikali kupata thamani halisi ya fedha zinazotumika kupitia ununuzi wa bidhaa.
Amesema taasisi za umma ambazo tayari zimeunganishwa katika mfumo wa ununuzi kwa njia ya kieletroniki ni jumla ya taasisi nunuzi 418 kati ya taasisi 540 sawa na asilimia 77.4 ya taasisi nunuzi zilizopo nchini zimeunganishwa na mfumo huo.
James amesema tangu kuanza kwa mfumo huo kumeongeza ushindani kwenye michakato ya ununuzi ,kuongeza ufanisi na hivyo kupunguza muda unaotumika katika michakato ya zabuni pamoja kuongeza uwazi hivyo kupunguza vitendo vya rushwa.
Kwa upande wake Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Kudhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA) Mhandisi Leonard Kapongo amesema baada ya kupewa maagizo na Serikali waliingia kazini kuongeza katika kutoa mafunzo kuhusiana na mfumo kwa maafisa Ununuzi na Tehama wa Taasisi za Umma.
Amesema hawataruhusu taasisi za umma kufanya nunuzi nje ya mfumo wa ununuzi kwa njia ya kieletroniki kufikia Januari 31 mwaka ujao.
Mhandisi Kapongo amesema taasisi ambazo hazjaunganishwa wajiunge ikiwa ni pamoja na kugharamia mafunzo maakumu ya namna ya kutumia mfumo wa ununuzi kwa njia ya kieletroniki.