Aliyekuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof. Mussa Assad, amesema hana kinyongo na mtu yeyote na sasa anajiandaa kurejea nyumbani kuendesha shughuli za kilimo na ufugaji wa kuku.


Pia mtaalamu huyo wa ukaguzi wa hesabu, amesema amesamehe wote waliomkwaza na kuomba asamehewe na kila aliyekwazwa naye, huku akisisitiza hajawahi kumtengenezea mtu jambo la kumuudhi katika maisha yake.

Prof. Assad aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam baada ya kuulizwa na Nipashe alipohudhuria mkutano wa sita wa Taasisi za Fedha za Kiislamu barani Afrika.

Juzi, Rais John Magufuli alimteua Charles Kichere kuwa CAG, akichukua nafasi ya Prof. Assad ambaye ilielezwa kuwa muda wake wa miaka mitano kuhudumu katika ofisi hiyo nyeti ulikuwa unafika kikomo saa sita usiku wa kuamkia leo.

“Hili suala (swali aliloulizwa kuhusu uteuzi mpya wa CAG) halihusiani na ‘summit’ (mkutano), ni suala la kibinadamu, nataka kusema, mimi katika mahusiano yote na watu wote, sijawahi kumkosea mtu kwa kudhamiria, sijawahi hata siku moja kumtengenezea mtu kumuudhi,” alisema.

Aliongeza kuwa kama kuna watu ilitokea akawaudhi, basi ni kwa sababu ya kusimamia misingi ya kazi.

“Nakumbuka niliwafukuza kazi kama watu wanne kwa sababu kulikuwa na wizi na ushahidi ulikuwapo na mmoja alikuwa ni rafiki yangu kabisa, alikuwa ananisaidia. Nilimfukuza kwa sababu kulikuwa na ushahidi wa wizi, watu kama hao wanaweza kunichukia kwa sababu ya kusimamia misingi,” alisema Prof. Assad.

Mwanataaluma huyo wa zamani wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alisema anafikiri kusamehe ni jambo muhimu kwa watu wote.

Alipoulizwa kuhusu mipango yake ya maisha baada ya kuondoka katika Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi, Prof. Assad alisema: “Sina ‘position’ (nafasi) yoyote kwa sasa, nipo kwenye kitu kinachoitwa maandalizi ya kustaafu, nimekaa nyumbani nikiwa nina (umri wa) miaka 58,” alisema.

Prof. Assad alisema kwa kuwa taratibu za nchi haziruhusu CAG kufanya kazi yoyote ya serikali baada ya kuondoka katika nafasi yake hiyo, atalazimika kurejea nyumbani kuendesha shughuli za kilimo na ufugaji.

“Ninakwenda kufuga kuku, tuna mashamba tumeyaanzisha, nina mambo mengi ya kufanya,” alisema.

Nipashe pia ilimuuliza msomi huyo kama ana ushauri kwa CAG mpya, akaeleza kuwa leo wakati wa kukabidhi ofisi, atatoa ushauri kwa mwanafunzi wake huyo.

“Kesho (leo) nitakutana na Kichere Dodoma, nitampatia ushauri wangu, yule ni mwanafunzi wangu, nilimfundisha,” alisema Prof. Assad.

Desemba Mosi, 2014, Ikulu ilitangaza kuwa Rais Jakaya Kikwete alikuwa amemteua Prof. Assad kuwa CAG na uteuzi wake ulikuwa umeanza tangu Novemba 5, mwaka huo.

Kabla ya uteuzi huo, Prof. Assad alikuwa Profesa Mshiriki, Idara ya Uhasibu, UDSM na alichukua nafasi ya Ludovick Utouh, ambaye alistaafu kwa mujibu wa Sheria za Utumishi wa Umma.

Ilielezwa kwenye taarifa ya Ikulu siku hiyo kwamba, Prof. Assad ni msomi, mwenye weledi, ujuzi na uzoefu mkubwa wa uhasibu na udhibiti wa fedha ambaye ana Shahada ya Uzamivu wa Uhasibu (PhD in Accounting) kutoka Chuo Kikuu cha Southampton, Uingereza mwaka 2001 na Shahada ya Uzamivu katika Udhibiti wa Fedha (MA in Financial Accounting) kutoka Chuo Kikuu cha Dublin City, Jamhuri ya Ireland mwaka 1991