Sherehe za kugawana faida katika kikundi cha ujasiriamali cha Imani, zilizokuwa zifanyike mapema mwishoni mwa wiki zimegeuka kilio kwa wanachama na wengine kuzimia ghafla ukumbini, baada ya taarifa ya upotevu wa zaidi ya Sh milioni 39, zinazodaiwa kuyeyuka kwa njia ya ushirikina.

Fedha hizo ziliyeyuka ndani ya sanduku la fedha nyumbani kwa Mweka Hazina wa kikundi cha watu 20.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha mmoja wa wanakikundi hicho chenye makao Ngusero kata ya Sombetini, Arusha, Grace Magala amesema kikundi chao chenye miaka mitano tangu kuanzishwa, hawajawahi kugawana faida yoyote hadi juzi walipokaa na kukubaliana kugawana faida.

Alieleza kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na katibu, Deogratius Seif, kikundi hicho hadi kuvunjwa juzi kilikuwa na faida ya zaidi ya Sh milioni 39 ambazo zingegawanywa kwa wanakikundi.

Katika hali ya sintofahamu, wanakikundi hao waliambiwa fedha hizo zimeyeyuka ndani humo katika mazingira ya kutatanisha jambo lililozua taharuki kwa akina mama waliokuwa wameambatana na waume zao ili kupokea gawio kwa lengo la kufanya manunuzi na mahitaji mengine ya majumbani.

“Tulihoji ni kwa nini fedha nyingine zipotee Sh. milioni 39 wakati nyingine zipo ndani ya sanduku, Katibu alitujibu fedha nyingine zipo mikononi mwa wanachama hivyo tusubiri mchakato unaendelea,” amesema.

Katibu wa kikundi hicho, Deogratius Seif amesema wanaendelea na ufuatiliaji na watakutana na viongozi wa kikundi kujua tatizo ndio watoe taarifa kamili kuhusu upotevu wa fedha au makosa ya kimahesabu.

Ijumaa wiki iliyopita wanakikundi hao walijikusanya ukumbi wa Shule ya Highview kupata gawio la faida ya michango yao lakini walishangaa Mweka hazina wa kikundi hicho, Halima Mwidadi kuwaeleza kuwa kulikuwa hakuna fedha zozote kwani zaidi ya Sh milioni 39 hazioni mahali alipozihifadhi nyumbani.

Akizungumzia suala hilo kwa simu, Mweka hazina huyo, Halima amesema bado anaendelea kufanya mahesabu vizuri ili kubaini kiasi cha fedha kilichopotea ila anakubaliana na upotevu huo.

Amesema hajui fedha hizo zimepotea kimazingira au ushirikina kwani sanduku halijavunjwa kokote.