Serikali kupitia Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) imeahidi kuendelea kusaidia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kijamii katika sekta za afya, elimu, maji na Mifugo kwa wakazi wanaoishi ndani ya Hifadhi hiyo.
Ahadi hiyo imetolewa na Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Dkt. Freddy Manongi wakati wa ziara yake ya kutembelea maendeleo ya miradi mbalimbali inayofadhiliwa na Hifadhi hiyo ikiwa ni adhma ya Serikali kuhakikisha kuwa wananchi hao kama sehemu ya hifadhi wananufaika na mapato yatokanayo na Utalii kwa kusaidia ujenzi wa miradi ya kijamii hususan elimu, afya, maji na huduma za Mifugo.
Dkt. Manongi ameeleza kuwa kupitia mpango wa kusaidia huduma za maendeleo kwa wakazi wanaoshi ndani ya Hifadhi hiyo , NCAA imesaidia Ujenzi wa Shule za Msingi zaidi ya 22, shule mbili za Sekondari, zahanati katika vijiji mbalimbali, miradi ya maji pamoja na chanjo za mifugo.
“Wakazi mnaoishi ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro ni sehemu ya wadau wa uhifadhi, kwa kutambua umuhimu huo Serikali yenu kupitia Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro itaendelea kutenga fedha katika mapato yake ya kila mwaka ili kusaidia ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo hasa kuwekeza katika elimu ya watoto wetu na kuwajengea mabweni ili kwa kuweka mazingira rafiki ya kusoma kutokana na jiografia ya maeneo ya wafugaji” ameeleza Dkt Manongi.
Ameongeza kuwa katika mwaka huu wa fedha 2019/2020 pamoja na miradi mingine iliyopangwa kutekelezwa tayari Mamlaka hiyo imepanga kutoa fedha kiasi cha shilingi milioni 10 mwezi Desemba, 2019 kama sehemu ya kusaidia ujenzi wa darasa na ununuzi wa madawati 50 katika shule ya msingi Olpiro iliyoko kata ya Eyasi ili kuwasaidia watoto wa jamii ya Wadatoga kusoma katika mazingira bora na kuhakikisha kuwa utaratibu wa utoaji wa huduma ya chakula kwa watoto wa shule hiyo unaendelea.
Kamishna Manongi amebainisha kuwa mpango wa muda mrefu wa Mamlaka hiyo ni kujenga Mabweni hasa kwa shule ambazo watoto wanatembea umbali mrefu ili kuwajengea wanafunzi mazingira mazuri ya kusoma kwa kukaa shuleni na kuepuka kutembea umbali mrefu kila siku.
Kamishina wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Dkt Freddy Manongi (katikati) akiongozana na watendaji mbalimbali wa Tarafa ya Ngorongoro na kata ya Eyasi wakati wa ziara yake ya kutembelea miradi mbalimbali inayofadhiliwa na Mamlaka hiyo.
Sehemu ya wananchi wa Kata ya Eyasi iliyoko ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro wakimsikiliza Dkt Manongi.
Dkt Freddy Manongi akiongea na watendaji pamoja na wananchi wa kata ya Eyasi kuhusu miradi mbalimbali ya kijamii inayofadhiliwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.