Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali imefanikiwa kukusanya mikopo iliyoiva yenye thamani ya shilingi bilioni 183.3 sawa na asilimia 116.2 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 157.7.

Ametoa kauli hiyo leo mchana (Ijumaa, Novemba 29, 2019) wakati akizungumza kwenye mahafali ya 45 ya Chuo cha Usimamizi wa Fedha yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam.

“Natambua kwamba baadhi ya wahitimu wamepata mkopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, hivyo natumia  fursa hii kuwakumbusha wale wote mlionufaika na mkopo wa Serikali katika kutimiza ndoto zenu za kupata elimu ya juu, mkumbuke kurejesha mikopo,” amesema.

Amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa kila anayenufaika na mkopo asaidie wengine walio nyuma yake ili nao waweze kufaidika na utaratibu huo wa kukopa na kulipa.

Alisisitiza  kwamba bila kufanya hivyo, ni ukweli usiopingika kuwa Serikali itashindwa kuwajengea uwezo wananchi wake wa kupata fursa zinazojitokeza za elimu katika ngazi
mbalimbali.

“Ikumbukwe kuwa, maendeleo ya Taifa lolote yanategemea uwekezaji katika rasilimali watu. Hivyo nitoe rai kuwa wote mliokopeshwa na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu mfanye hima kulipa,” amesema Majaliwa