Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe (katikati) akipata maelezo kutoka kwa Mkufunzi Msaidizi wa Chuo kikuu cha Dodoma, Jabhera Matogoro (wa kwanza kushoto) aliyebuni teknolojia ya kutumia mawimbi ya luninga kupeleka huduma ya intaneti kwenye jamii akiwa ziarani wilayani Kondoa, Dodoma.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe akisisitiza jambo baada ya kutoka kukagua mnara wa mawimbi ya luninga yanayotumika kupeleka huduma ya intaneti kwenye Jamii ya Mtandao wa Intaneti Kondoa (KCN) akiwa wilayani Kondoa, Dodoma. Wa kwanza Kulia ni Katibu Mkuu wa Mawasiliano, Mhandisi Dkt. Maria Sasabo.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe (hayupo pichani) akiangalia Kifaa (kinachooneka pichani) kinachobadilisha mawimbi ya luninga kuwa ya intaneti ili kutoa huduma ya intaneti kwenye shule ya Sekondari ya Wasichana ya Kondoa iliyopo wilayani humo, Dodoma kabla ya kufunga Kongamano la Nne la Mitadao Jamii lililofanyika shuleni hapo.
Baadhi ya wataalamu wa TEHAMA kutoka nchi 18 duniani wakiandika kwenye simu zao maelekezo anayotoa Waziri wa Ujenzi, uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe (hayupo pichani) wakati akifunga Kongamano la Nne la Mitandao Jamii lililofanyika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Kondoa, Dodoma.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe (wa pili kulia) akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Kondoa (hawapo pichani) baada ya kufunga Kongamano la Nne la Mitandao Jamii lililofanyika wilayani Kondoa, Dodoma. Wa kwanza kulia ni Katibu wa Wizara hiyo (Sekta ya Mawasiliano) Mhandisi Dkt. Maria Sasabo.

Na Prisca Ulomi, Kondoa.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe ameelekeza mawimbi ya luninga yatumike kupeleka huduma ya intaneti vijijini ili jamii iweze kutumia mawimbi hayo kupata huduma ya mawasiliano ya intaneti.

Kamwelwe ameyasema hayo wakati akikagua mnara wa mawasiliano, Kondoa mjini ambao umefungwa vifaa maalumu kwa ajili ya kubeba mawimbi ya luninga na kupeleka kwenye kifaa kingine ambapo mawimbi hayo yanabadilishwa na kuweza kutumika kutoa huduma ya intaneti kwenye jamii ya shule ya sekondari ya Wasichana ya Kondoa, shule ya sekondari ya Ura na Chuo cha Ualimu cha Bustani zilizopo wilayani Kondoa, Dodoma.

Kamwelwe alipita kukagua mnara huo na teknolojia hiyo kabla ya kufunga Kongamano la Nne la Mtandao wa Intaneti kwenye Jamii lenye kauli mbiu isemayo, “Kuunganisha Wananchi Kimtandao”. Kongamano hilo limefanyika kwa muda wa siku 6 kwenye Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na kwenye Shule ya Sekondari ya Wasichana Kondoa ambalo lilianza tarehe 28 Oktoba 2019 na kumalizika tarehe 2 Novemba, 2019.

Wakati Kamwelwe akikagua mnara huo, Mkufunzi Msaidizi wa UDOM, Jabhera Matogoro alimweleza Kamwelwe kuwa mawimbi kwa ajili ya luninga yanasafiri umbali wa kipenyo kizichozidi kilomita ishirini ambapo baadhi ya maeneo hayafikiwi na mawimbi hayo ambapo kiasi kikubwa cha mawimbi yanabaki bila kutumika ipasavyo.

Matogoro aliongeza kuwa, watoa huduma wanapatiwa leseni ya kurusha mawimbi hayo kwenye Wilaya au Mkoa husika ambapo imebainika kuwa kiasi kidogo cha mawimbi hayo ndio kinachotumika kwa ajili ya kurusha matangazo ya luninga na mawasiliano ya simu za mkononi.

Alifafanua zaidi kuwa, katika utafiti wake, amebaini kuwa mawimbi hayo yanaweza kubadilishwa kwa kutumia vifaa maalumu kwa kuzingatia ukuaji na maendeleo ya teknolojia ambapo mawimbi ya luninga yanaweza kutumika kupeleka huduma ya intaneti katika jamii husika.

“Lengo kuu ni kuunganisha jamii na wananchi ambao hawajaunganishwa na mtandao wa intaneti kwa kutumia mawimbi ya luninga”, amesisitiza Matogoro .Kamwelwe amempongeza Matogoro na kubatiza utafiti wake jina la “Teknolojia ya Matogoro” (Matogoro Technology) kwa kuwa amebuni teknolojia hiyo ya kutumia mawimbi ya luninga kupeleka huduma ya intaneti kwenye jamii na kumuahidi kuwa Serikali itahakikisha teknolojia hiyo inatumika na kuenea sehemu mbali mbali nchini.

“Mwenye sera, sheria na kanuni zinazohusu Sekta ya Mawasiliano ni mimi, nitakaa na taasisi na wataalamu ili ikibidi tuzibadilishe ili kuhakikisha kuwa mnaendelea kuongeza matumizi ya mawimbi ya luninga kutoa huduma ya intaneti kwenye jamii” amesisitiza Kamwelwe.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya
Mawasiliano) Mhandisi Dkt. Maria Sasabo, amesema kuwa maelekezo ya Kamwelwe yamezingatiwa ya kuhakikisha kuwa TEHAMA inaendelea kuchangia maendeleo ya taifa, ukuaji wa uchumi wetu na kuwezesha utoaji na upatikanaji wa huduma za kijamii.

Pia, Kamwelwe ameuelekeza uongozi wa UDOM kuwasilisha maombi rasmi ofisini kwake ili waweze kupewa kibali kwa ajili ya mtafiti na mtaalamu wao kuweza kuendelea kutumia mawimbi hayo kutoa huduma ya intaneti kwenye taasisi hizo.

Mwakilishi wa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha UDOM Prof. Leonard Masele,amemshukuru Kamwelwe kwa kufika na kuona Mtandao wa Intaneti wa Kondoa na amemuomba kumpatia kibali Matogoro cha kuendelea kutumia teknolojia hiyo kwenye taasisi hizo ili ziweze kuendelea kunufaika na huduma ya intaneti.

Naye mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, Ally Mbena amemshukuru mtaalamu wa UDOM kwa kuchukua hatua za kutatua changamoto za kijamii na huu ndio usomi.

Kiongozi wa taasisi ya kidunia ya Association for Progressive Communication, Prof. Carlos Rey-Moreno amesema kuwa sio nchi zote za Afrika zinachukulia suala la mawasiliano ya kielektroniki kama huduma ya msingi na sio biashara kama ilivyo huduma ya maji na umeme.

Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Kondoa amesema kuwa mtandao wa intaneti umeiweka Kondoa na Tanzania kwenye ramani ya dunia na umewasaidia kuongeza kiwango cha ufaulu, kupata maarifa mbali mbali na bila kulipia gharama yeyote.

Kongamano hilo limehudhuriwa na wataalamu wa taasisi za Serikali na binafsi 135 kutoka nchi 18 ikiwemo Argentina, Canada, Hispania, Uingereza, Marekani, DRC Congo, Cameroon, Ethiopia, Kenya, Malawi, Namibia, Nigeria, Afrika Kusini, Uganda, Zimbambwe, Ujerumani, Ufaransa, na Tanzania