KATIKA toleo la Gazeti la Spoti Xtra Alhamisi iliyopita, Marioo alianza kuelezea historia ya maisha pamoja na kazi yake ya muziki ilivyoanza. Marioo ambaye jina lake kamili ni Omary Ally Mwanga ni miongoni mwa wasanii chipukizi ambaye kwa sasa analiteka soko la Muziki wa Bongo Fleva.



Nikukumbushe tu kuwa, Marioo alipata vikwazo vingi katika safari yake ya muziki wakati huo akiwa anafanya kazi gereji. Leo Marioo anaendelea kusimulia sehemu hii ya mwisho ambapo anatueleza namna alivyokutana na prodyuza Abbah hadi kufikia hatua ya kufanya naye ngoma mbili ikiwemo Chibonge.



Marioo ni mtoto wa tatu katika familia yao ya watoto wanne ambapo watoto watatu ni wa baba mmoja na mmoja wamechangia mama tu.



“Kwa ufupi mimi na Abbah tulikutanishwa na rafiki yangu mmoja itwaye Tonch Master ambaye ni kaka yangu ninayemuheshimu sana hasa nikizungumzia safari hii ya muziki wangu. “Tonch Master siku ya kwanza nilikutana naye nilipoenda studio kwa Abbah, siku hiyo Abbah hakuwepo ndipo nikapokelewa na Tonch Master.



“Nilimueleza Tonch Master nia yangu ya kufika pale nilikuwa nataka kufanya ngoma, lakini akaniambia wao wana rekodi kwa shilingi laki tatu, nikamlilia anipunguzie, akakubali kunifanyia kwa shilingi laki moja na nusu.



“Hata hiyo shilingi laki moja na nusu sikumlipa yote, nikamlipa nusunusu. Ilipotimia ndiyo nikaenda kurekodi.



“Siku niliyoenda kurekodi, niliwahi sana, nikakaa nje pale wao walikuwa bado hajaamka, walipoamka nikachukua ufagio nikafagia, pia nilikuta umeme umeisha, nikanunua ilimradi tu nirekodi. “Baada ya kumaliza yote hayo, Tonch Master alinipa biti moja ambayo alikuwa ameitengeneza Abbah, nikaimba wimbo unaoitwa Mboni Yangu.



“Nilipomaliza kuingiza sauti, akaniambia ataufanyia mixing lakini pia akaniomba nimalizie shilingi elfu hamsini iliyobaki, kisha akaniambia siku fulani niende kuusikiliza utakuwa tayari.



“Siku niliyoenda, sikusikia chochote, lakini nilipokuwa hapo studio, nikasikia watu wakiuimba, kumbe tayari Abbah alikuwa ameshausikia. Akaniambia ataufanyia mixing.



“Kuanzia hapo akaniambia nitakuwa nafanya kazi zangu pale, nikaendelea kufanya ngoma zote kwa Abbah, akaahidi kunisaidia hivyo nikawa nakaa na kulala palepale.



“Wakati bado naendelea kuhangaika kutoka, kuna siku Abbah alikutana na Dully Sykes, akamsikilizisha ngoma yangu, akaomba kuniona.



“Nilipokutana na Dully, akaukubali uwezo wangu, nikawa nakaa kwake, lakini baadaye akawa bize sana akashindwa kunisaidia zaidi. “Nikaja kukutana na Gala Tone, baadaye nikaenda kwa prodyuza Bonga ambako napo nilitumia muda mwingi sikutoka, nikapelekwa kwa Emma the Boy pale THT.



“Huko kote nikawa kama natembea tu, nikarudi kwa Abbah, nilipelekwa tena hapo na Kapasta, Abbah akawa ana mambo mengi, Kapasta akaniomba niwe nawaandikia wimbo baadhi ya wasanii.



“Kuna siku akaniomba nimuandikie wimbo Nandy, lakini Nandy akanidharau. Sikujali.

“Nikaifanya kazi yangu, nikamsikilizisha Nandy ule wimbo akaukubali, kuanzia hapo akanikubali sana. “Katika harakati hizo, ndiyo tukafanya ngoma na Abbah ile Chibonge kwa sababu tayari Abbah alikuwa ameshauelewa uwezo wangu.



KUANDIKA NA KUIMBA KIPI KINAKUINGIZIA SANA FEDHA?

“Kwa sasa naweza kusema kuimba inaniingizia fedha nyingi kwa sababu zile ishu za kuwaandikia wasanii nimeacha, nimejikita zaidi katika kuimba nyimbo zangu na tayari kuna nyimbo kadhaa zipo tayari zinasubiri kutoka tu.



VIPI KOLABO NA ALIKIBA AU DIAMOND?

Kolabo na wasanii wakubwa kama Alikiba na Diamond nitafanya muda ukifika, ila kwa mwaka huu kuna kolabo moja matata ambayo wimbo wake utatoka siku si nyingi mashabiki wangu wakae mkao wa kula,” anamaliza Marioo.