Na Magreth Kinabo- Mahakama
Mahakama ya Wilaya ya Ilala, iliyopo Kinyerezi, jijini Dar es Salaam, imepanga kumaliza mashauri 150 kati ya 194 ya mlundikano ifikapo Desemba 30, mwaka huu.

Hayo yamesemwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo leo, Mhe. Martha Mpaze Novemba 27, mwaka huu, wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi, jijini Dar es Salaam.

Ambapo alisema mashauri hayo yaliyozidi umri wa miezi 12 ni ya madai na jinai, hivyo ambayo wana mamlaka nayo ni 150, na yasio na mamlaka nayo ni 44 kwa kuwa ni ya mauaji yanahitaji kusikilizwa na Mahakama Kuu ya Tanzania.

Aliongeza kwamba mashauri hayo 150 kila hakimu atasikiliza mashauri nane kwa kuwa hivi wana idadi ya mahakimu 18.

Mpaze alitaja sababu za mashauri hayo kuzidi umri ni baadhi ya mashahidi kutofika mahakamani kwa wakati na kuwepo kwa waendesha mashtaka wachache.

Aidha Mhe. Mpaze alifafanua kuwa Mahakama hiyo kwa mwaka inasajili mashauri 3,335.

Alisema katika kipindi cha mwaka 2018, Mahakama hiyo ilisajili mashauri 3,038 katika kipindi cha mwezi Januari hadi Oktoba, ambapo mashauri 2,624 yalimalizika, wakati katika kipindi hicho pia mwaka 2019 mashauri 2,812 yalisajiliwa na yaliyomalizika ni 2,973.mashauri. Mashauri yaliyobakia kwa mwaka 2018 ni 1,491na mwaka 2019 ni 1,456. Mahakama hiyo ilizinduliwa rasmi Februari 6, mwaka 2019
 Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Ilala , Mhe. Martha Mpaze (aliyevaa blauzi ya bluu) akizungumza jambo kuhusu mahakama hiyo na majaji wapya wa Mahakama Kuu ya Tanzania waliapishwa hivi karibuni.
Mahakama ya Wilaya ya Ilala.