Mwanga umeonekana katika mgogoro wa muda mrefu wa Kisiwa cha Migingo baada ya Kenya na Uganda kutia saini makubaliano ya kukitumia kwa kushirikiana.

Hata hivyo, makubaliano hayo yamefanyika huku Kenya ikiendelea kusisitiza kuwa kisiwa hicho ni sehemu ya ardhi yake.

Tovuti ya Gazeti la The Daily Nation imemnukuu waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Monica Juma akisema makubaliano hayo yamefanyika na Kenya na mamlaka za Uganda ili kuruhusu wavuvi kutumia upande wowote wa kisiwa hicho.

Alisema kilichosalia sasa ni kuweka taratibu za namna ya kushirikiana katika uendeshaji na rasilimali za kisiwa hicho chenye ukubwa wa mita za mraba 2,000.

“Wakenya wanatakiwa kufahamu kuwa hii mipaka inatumika kwa ushirikiano wa jamii hivyo tunatakiwa kuweka masharti mepesi.

“Ujumbe wangu kwa Wakenya kwamba tunatanguliza maslahi yao na hii inaweza kuthibitika jinsi tunavyopungua athari wanazokumbana nazo katika kutumia rasilimali za nchi,” aliongeza waziri huyo.

Alipoulizwa iwapo makubaliano hayo yataeleza ni nani mmiliki wa kisiwa hicho, Waziri Juma alisema: “ Wakenya wanatakiwa kufahamu kuwa mipaka ya nchi kamwe haiwezi kujadiliwa na kuwekewa makubaliano.”

Kenya kwa muda mrefu imekuwa ikiilaumu Uganda kuwa wanajeshi wake wamekuwa wakiwanyanyasa Wakenya wanaokwenda kwenye kisiwa hicho.

Kisiwa hicho kimekuwa chanzo cha mvutano kati ya Kenya na Uganda kwa zaidi ya miaka kumi iliyopita, huku kila nchi ikidai ni mali yake.

Februari 2017 kikosi maalum cha Jeshi la Uganda (SFC) chenye jukumu la kumlinda Rais Yoweri Museveni kilipelekwa kwenye kisiwa hicho ili kudhibiti uvuvi haramu.