Jumuiya ya Afrika Mashariki imesaini mkataba wa EURO milioni 10 na umoja wa nchi za Ulaya kwa ajili ya kuimarisha ulinzi na usalama katika nchi uanachama wa jumuiya hiyo.
Mkataba huo umesainiwa jana katika ofisi za makao makuu ya jumuiya hiyo na Katibu mkuu wa jumuiya ya Afrika Mashariki ,Liberat Mfumukeko na Balozi wa umoja wa nchi za Ulaya Tanzania ,Manfredo Fanti.
Akizungumza wakati wa kusaini mkataba huo ,Katibu mkuu wa EAC ,amesema kuwa, fedha hizo zimetolewa na jumuiya ya umoja huo ili kuziwezesha nchi wanachama kukabiliana na changamoto ya usalama ambayo imekuwa na kikwazo kikubwa Cha maendeleo katika nchi hizo.
Ameshukuru jumuiya hiyo kwa msaada huo ambao umekuja muda muafaka na kuongeza kuwa, jumuiya hiyo itaendelea kushirikiana kwa ukaribu Sana katika nyanja mbalimbali za maendeleo.
Hata hivyo ,Mfumukeko amesema kuwa,jumuiya hiyo ya nchi za Ulaya wamekuwa washirikiana kwa muda mrefu na jumuiya hiyo ambapo katika kipindi cha miaka mitano wamekwisha kutoa kiasi Cha EURO milioni 85 .
“Umoja wa Ulaya wamekuwa washirika muhimu katika kusukuma mbele ajenda ya mtangamano wenye lengo la kuwawezesha kiuchumi, ipo miradi mbalimbali ambayo imefadhiliwa na EU tangu mwaka 2007 ambayo imekua na matokeo chanya kwa wananchi wetu.
“Programu hii ambayo tumeizindua itasaidia kupunguza nafasi ya kushamiri kwa uhalifu unaovuka mipaka ya nchi moja kwenda nyingine ambayo unaweza kutishia mchakato wa mtangamano, pia itasaidia kuendeleza sera na utekelezaji wake, uwajibikaji kisiasa na uimarishaji wa taasisi,” amesema Mfumukeko.
Kwa upande wake ,Balozi wa jumuiya ya umoja wa Ulaya nchini Tanzania,Manfredo Fanti amesema kuwa, wataendelea kusaidia jumuiya hiyo katika maswala mbalimbali ya maendeleo .
“Tumekuwa tukisaidia jumuiya ya Afrika Mashariki katika miradi mbalimbali tangu mwaka 2007 ambayo imeleta manufaa makubwa kwa wananchi wa nchi hizo na kuondokana na changamoto mbalimbali zinazowakabili.”amesema Balozi huyo.