Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Juma amefanya ziara ya siku Moja Mkoani Songwe na kumkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela Mpango wa Miaka mitano wa maendeleo ya Miundombinu ya Mahakama ya Tanzania.

Makabidhiano hayo yamefanyika mepama leo katika Ofisi ya Hakimu wa Mkoa wa Songwe iliyopo Vwawa ambapo Profesa Juma amesema Mpango huo utamwezesha Brig. Jen. Mwangela kusaidia kusukuma na kufuatilia utekelezaji wake.

Profesa Juma amesema ziara yake imelenga kuona Changamoto ambazo Mahakama inazo kwa Mkoa wa Songwe na kwakuwa Mkoa huu ni Mpya, wameuweka katika mipango yao kwakuwa kila sehemu yenye changamoto imewekewa ratiba ya utekelezaji.

“Bila kuweka Mpango Mkakati na kupanga lini unafanya nini, utajikuta hakuna chochote kitakacho onekana kinafanyika, kwahiyo ninakukabidhi Mpango wa Miaka Mitano wa Maendeleo ya miundombinu ya Mahakama ya Tanzania, si kwa hapa Mkoani tu hadi katika Wilaya za Mkoa wa Songwe.”, amesema Profesa Juma.

Katika ziara yake Profesa Juma ametembelea Mahakama ya Mwanzo ya Mlowo, amekagua eneo itakapojengwa mahakama ya Mkoa katika kijiji cha Selewa Wilayani Mbozi na kutembelea Mahakama ya Mkoa iliyopo Vwawa.

Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela amemshukuru Profesa Juma kwa kutembelea Mkoa wa Songwe na ana matuamini kuwa Miundo mbinu ya Mhakama Mkoani hapa itaboreshwa.
 Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela akisalimiana na Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Juma (mwenye tai nyekundu) mapema leo katika eneo la Mahakama ya Mwanzo Mlowo.
 Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela akionyesha Kitabu cha Mpango wa Miaka mitano wa maendeleo ya Miundombinu ya Mahakama ya Tanzania ambacho amekabidhiwa mapema leo na Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Juma.
Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Juma (mwenye tai nyekundu) akikagua ramani ya eneo ambapo itajengwa Mahakama ya Mkoa katika kijiji cha Selewa Wilaya ya Mbozi mapema leo alipotembelea Mkoa wa Songwe.