Mwakililishi wa Shirika la Kimataifa la Chakula na Kilimo (FAO) nchini Tanzania, Fred Kafeero (wa kwanza kushoto) akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu umuhimu wa kilimo hai nchini Tanzania.Katikati ni Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania FrÈdÈric Clavier.
Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, FrÈdÈric Clavier akizungumza wakati wa mkutano walipozungumzia mkutano mkuu wa wadau wa Kilimo hai. Kushoto ni Mwakililishi wa Shirika la Kimataifa la Chakula na Kilimo (FAO) nchini Tanzania Fred Kafeero na Mkuu wa Ushirikiano na Masuala ya Utamaduni ubalozini, Cecile Frobert.
Mshauri wa Mawasiliano Shirika la kuendeleza Kilimo hai nchini Tanzania(TOAM), Costantine Akitanda akizungumza wakati wa mkutano walipozungumzia mkutano mkuu wa wadau wa Kilimo hai.Wapili kushoto ni Mwakililishi wa Shirika la Kimataifa la Chakula na Kilimo (FAO) nchini Tanzania, Fred Kafeero na Mkuu wa Ushirikiano na Maswala ya Utamaduni ubalozini, Cecile Frobert.
Na Said Mwishehe, Globu ya jamii.
KILIMO Hai chenye kuzingatia misingi ya Ikolojia ni moja ya vipaumbele muhimu vya Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) na kwamba aina hiyo ya kilimo mbali ya kuwawezesha wakulima kuhimili changamoto mbali mbali ikiwemo mabadiliko ya tabia nchi na pia ni rafiki kwa mazingira kwa kuzingatia utegemezi wa viumbe vyote yaani mimea, wanyama, binadamu na mazingira yao.
Hayo yamesemwa leo Novemba 13, mwaka 2019 jijini Dar es Salaam na Mwakilishi wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa(FAO) nchini Tanzania Fred Kafeero wakati wa mkutano wa waandishi wa habari uliohusisha pia ofisa wa Shirika la Kuendeleza Kilimo Hai nchini(TOAM) na Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Frederic Clavier.
Mkutano huo umeitishwa ikiwa ni kuelezea hatua mbalimbali kuelekea Mkutano Mkuu unaotarajiwa kufanyika Novemba 26 hadi Novemba 27 mwaka huu Mjini Dodoma ambapo wadau mbalimbali wa kilimo hai pamoja na viongozi wa serikali wanaohusika wa kilimo watakutana kujadili masuala mbalimbali yanayohusu kilimo hai ikiwa pamoja na kutafuta ufumbuzi wa changamoto zilizopo.
Akizungumza zaidi Mwakilishi wa FAO nchini Tanzania Kafeero amesema kuwa Mkutano huo mku wa wadau wa kilimo hai hapa nchini utakuwa ni jukwaa muhimu la majadiliano na kubadilishana mawazo na mbinu za kuimarisha aina hiyo ya kilimo nchini.
"Unakuja wiki mbili tu baada ya FAO pamoja na Shirika la Kuhamasisha Kilimo Hai hapa nchini (TOAM) kutoa mafunzo ya kilimo hai chenye kuheshimu misingi ya ikolojia kwa zaidi ya waandishi 20 kutoka vyombo mbali mbali vya habari hapa nchini yaliyofanyika Moshi mkoani Kilimanjaro.
"Wanahabari hawa, ambao wanategemewa kuwa chachu katika kuhamasisha kuhusu kilimo hai hapa nchini, pia walipata nafasi ya kutembelea shamba lililopo kwenye mfumo wa kilimo wa ‘Kihamba’ miongoni mwa kabila la Kichaga, ambao ni sehemu ya Mradi Kutambua na Kuenzi Mifumo ya Asili ya Uzalishaji uliofadhiliwa na FAO,"amesema. Amesema kilimo hai ni njia salama na endelevu ya uzalishaji wa chakula kwa sasa na kuitaika jamii ya Watanzania kuwa mabalozi wa kukihamasisha hapa nchini.
Kuhusu changamoto ya bei ya mazao ya kilimo hai , Kafeero amesema kuwa hiyo si changamoto ya wakulima wa Tanzania tu bali ni tatizo la wakulima wote na hiyo inatokana na kusekana kwa sauti ya pamoja kutoka kwa wakulima kuhusu bei wanayoihitaji katika mazao yao ambayo yanatokana na kilimo hai.
Kwa upande wake Mtaalam Mshauri wa Mawasiliano kutoka ka Shirika la Kuendeleza Kilimo Hai Tanzania(TOAM)Costantine Akitanda amesema kuwa kilimo hai ni ajenda ya bara la Afrika kwa miaka 50 ijayo kuanzia mwaka 2013/2014 marais wa Bara hili la Afrika walikubaliana kuhusu ajenda 2063 ambayo inajikita katika mambo saba mpaka nane ya msingi.
Amesema katika mambo hayo yanayoihusu Tanzania , pamoja na eneo la kilimo hai ambayo inajielekeza katika mambo sita yakiwemo ya kufanya utafiti na kufundisha maofisa ugani ili kujikita kufanya kilimo hai katika misingi yenye kuleta tija."Kilimo hai n mchanganyiko wa kiasili na kisayansi na hivyo kunahitajika tafiti katika kukiendeleza na hasa kwa kutambua Tanzania sio kisiwa , hivyo nasi tunakwenda na tafiti ili kukifanikisha,"amesema Akitanda.
Kuhusu mkutano huo wa utakaofanyika Dodoma , Akitanda amesisitiza kuwa kuna mambo mengi ambayo wadau wa kilimo hai watajadiliana kwa pamoja na imani yao kuwa utatoa muelekeo mzuri zaidi wa nini kifanyike kuhakikisha kilimo hicho kinapewa nafasi kubwa hasa kwa kutambua ni kilimo ambacho kinatija kwa mkulima kutokana na soko la uhakika.
Akujibu swali kuhusu bei mazao ya kilimo hai, amejibu kuwa kuna mambo mengi ya kufanya lakini kubwa ni kuhakikisha kunakuwa na mawasiliano mazuri kati ya wadau na wakulima wa kilimo hicho."Ukweli ni kwamba mazao ya kilimo hai yanalipa kwani soko lake ni la uhakika sana.
"Duniani kote mazao yatokanayo na kilimo hai yamekuwa yakipata soko la uhakika na kwa bei nzuri.Nitoe mfano tu kahawa inatokana na kilimo hai bei yake iko juu na tunao mfano kule Arusha wakulima wa kahawa wana ushirika wao na wanauza kahawa yao kwa bei nzuri,"amesema Akitanda.
Wakati huo huo Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Frédéric Clavier ameeleza namna ambavyo wanafurahishwa na jitihada za Serikali ya Tanzania katka kuendeleza sekta ya kilimo na ushiriki wao katika kilimo hai. "Kilimo hai ni kilimo ambacho kinatunza mazingira na mazao yake ni bora na kwamba katika mkutao wa Dodoma watazungumzia changamoto zinazojitokeza kutokana na mabadiliko ya tabianchi yanayotokana na uharibu wa kimazingira,"amesema.
Balozi Clavier ameongeza kuwa kutokana na ushirikiano uliopo umesababisha nusu ya mamilioni ya wakulima Tanzania wametambulika kujihusisha na kilimo hai na hivyo kujihakikisha soko la uhakika. Pia amesema kwa sasa Watanzania wanahitaji kula vyakula vyenye ubora na vyenye kuongeza afya mwilini na mahitaji yatokanayo na kilimo hai yameongezeka katika soko la dunia huku akitolea mfano nchi za Asia, Ulaya, India na hiyo kunafursa kubwa kwa Watanzania kujalisha kwa wingi mazao ya kilimo hao na kupeleka katika nchi hizo.