Baada ya kuonekana akila bata nje ya nchi kila kukicha huku kazi zikiwa hazitoki wala kufanya shoo, staa wa Bongo Fleva, Omary Nyembo ‘Ommy Dimpoz’ ameibuka na kueleza siri yake.



Akizungumza na Gazeti la Ijumaa, Dimpoz alisema safari zake huwa ni za kikazi na wala siyo starehe kama watu wengi wanavyodhani hivyo waache kuzungumza vitu wasivyovijua.



“Siku zote katika maisha, watu hupenda kuzungumza mambo ambayo hawayajui kwani mara nyingi hawapendi kujua ukweli, ila ukweli ni kwamba mimi ni ‘brand’ na ninajitambua hivyo kupata safari nyingi nje ya nchi ni kawaida tu, watu waache kuongea sana.



“Mara nyingi huwa napata mialiko ya kazi kutoka kwa watu mbalimbali ya kwenda nje na huwezi kuamini kuna mingine hadi ninaikataa kwa sababu ya ratiba zangu kubana,” alisema Dimpoz ambaye anajulikana kwa kula bata kwenye viwanja vya mastaa wakubwa duniani kama Marekani na Ulaya.



Kwa upande mwingine aliwataka mashabiki wake kuondoa hofu kuhusiana na kutoa kazi kwani hivi karibuni anatarajia kuachia wimbo mpya, hivyo wampe sapoti.