Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) wametembelea na kutoa elimu  kwa wateja wapya wa Mkoa wa Kihuduma Kisarawe.

Mradi wa maji wa Kisarawe umekamilika mwanzoni mwa mwezi huu na tayari wateja wameshaunganishiwa huduma ya maji safi.

Meneja wa Dawasa mkoa wa kihuduma Kisarawe Erasto Mbwambo ameambatana na Meneja mawasiliano Everlasting Lyaro na Meneja huduma kwa wateja Doreen Kiwango kuwatembelea na kutoa elimu ya maji kwa wateja wa mji wa kisarawe waliokwisha unganishiwa huduma ya Majisafi baada ya kukamilika kwa mradi wa Maji wa Kibamba-Kisarawe

 Akizungumzia ziara hiyo, Meneja huduma kwa wateja Doreen Kiwango amesema lengo la kuwatembelea wateja wapya ni kuwatambua, kutoa elimu ya mambo mbalimbali yahusuyo huduma ya maji ikiwa ni pamoja na bili za kila mwezi, jinsi ya kulipa, namna wanaweza kutoa taarifa pindi wanahitaji msaada wa Dawasa na mambo mengi yanayofanana na hayo

"Hawa wateja ni wapya na kama Mamlaka tumeona umuhimu wa kuja kuongea nao, kujua namna walivyopokea huduma ya Maji na changamoto za awali wanazokutana nao kwenye ugeni huu wa maji mabombani" amesema kiwango

Kwa upande wake Meneja wa Dawasa Kisarawe, Erasto Mbwambo amesema mpaka sasa zaidi ya wateja 300 wameshafungiwa huduma huku nguvu kubwa ikielekezwa kwa wateja wakubwa na taasisi za serikali kama vile Hospitali, shule za sekondari na msingi, mahakama na sehemu nyingine ambazo huduma ya maji ni muhimu sana.

"Tunaenda vizuri, maombi ya wateja ni mengi sana na kiwango tulichonacho kuwafungia maji ni kikubwa pia.  Mpaka sasa tumejitahidi kufunga Maji kwanza kwenye makazi ya mkuu  wa wilaya na watendaji wengine wa ngazi za wilaya.  Hivyo tunaendelea na wananchi wa kawaida na taasisi za umma na binafsi zilizoleta maombi ya huduma, "amesema Mbwambo

Nae meneja mawasiliano wa Dawasa, Everlasting Lyaro alimalizia kwa kuwataka wananchi waliopata huduma ya Maji kuwa wazalendo na mabalozi wazuri wa mradi huu kwa kulinda na kutunza miundombinu ya maji ili iwafae jamii yote kwa miaka mingi zaidi.

"Mradi huu umetekelezwa na serikali ya Jamhuri ya Muungano kupitia Dawasa hivyo ni hela ya watanzania, tungependa sisi kama Mamlaka kuona mradi huu unatunzwa ili hata watoto wadogo wanakuja kuuona na kufurahi. Yoyote atakayekuwa chanzo cha uharibifu wa mradi huu tafadhali mtoe taarifa kwenye vyombo vya dola na DAWASA yenyewe "amesema Lyaro

Mradi wa Kisarawe  ulianza kutekelezwa mwezi Julai 2018, ukigharimu bilion 10.6 za kitanzania zikiwa ni fedha za ndani za DAWASA, mradi huo umehusisha ujenzi wa tanki la maji la Lita Milioni 6 na utahudumia wakazi wa Kisarawe na Vitongoji vyake pamoja na maeneo ya viwanda na hilo likiwa ni agizo la Rais Dkt John Pombe Magufuli alipokuwa anazindua mtambo wa Ruvu Juu.
Meneja huduma kwa wateja Doreen Kiwango DAWADA Doreen Kiwango( kulia)  akiwa na Meneja mawasiliano Everlasting Lyaro wakikagua mita ya maji sambamba na bomba la maji alilofungiwa mteja Mpya keenye mradi wa maji Kisarawe.
Meneja wa Mawasiliano wa Dawasa Everlasting Lyaro akikabidhi kipeperushi kwa mteja aliyeunganishiwa maji akiwa ameambatana na Meneja wa Dawasa mkoa wa kihuduma Kisarawe Erasto Mbwambo (kulia) na Meneja huduma kwa wateja Doreen Kiwango baada ya  kuwatembelea na kutoa elimu ya maji kwa wateja wa mji wa kisarawe waliokwisha unganishiwa huduma ya Majisafi baada ya kukamilika kwa mradi wa Maji wa Kibamba-Kisarawe
Meneja wa Dawasa mkoa wa kihuduma Kisarawe Erasto Mbwambo (katikati) akiwa na Meneja mawasiliano Everlasting Lyaro (kulia) na Meneja huduma kwa wateja Doreen Kiwango baada ya  kuwatembelea na kutoa elimu ya maji kwa wateja wa mji wa kisarawe waliokwisha unganishiwa huduma ya Majisafi baada ya kukamilika kwa mradi wa Maji wa Kibamba-Kisarawe