Mwenyekiti wa Bodi ya DAWASA Jenerali Mstaafu Davis Mwamunyange akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutembelea mradi wa maji wa Kisarawe uliokamilika kwa asilimia 99 na kufikia kesho wananchi wa Kisarawe wataanza kutumia maji safi na salama.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam DAWASA Mhandisi Cyprian Luhemeja (Kushoto) akitoa maelekezo kwa Kaimu Mkurugenzi wa Miradi na Uwekezaji DAWASA Mhandisi Ramadhan Mtindasi wakati wa ziara ya Mwenyekiti wa Bodi wa DAWASA Jenerali Mstaafu Davis Mwamunyange alipotembelea mradi huo uliopo kwenye hatua za mwisho
 Mwenyekiti wa Bodi DAWASA Jenerali Mstaafu Davis Mwamunyange (wa pili kushoto) akipanda ngazi kuelekea juu ya tanki la Kisarawe akiwa ameongozana na Afisa Mtendaji Mkuu DAWASA Mhandisi Cyprian Luhemeja na watendaji wengine wa Mamlaka hiyo. Picha ya chini akiwa juu ya tanki hilo.
 Msimamizi wa Mradi wa Kisarawe Mhandisi Ishmael Kakwezi akitoa maelezo kwa Mwenyekiti wa Bodi DAWASA Jeneral Mstaafu Davis Mwamunyange alipofika kuangalia kazi inayofanywa ya kuziba bomba linalovuja linalopeka maji Kisarawe.
Kaimu Mkurugenzi wa Miradi Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira DAWASA Mhandisi Ramadhan Mtindasi akitoa maelezo kwa Mwenyekiti wa Bodi DAWASA Jenerali Mstaafu Davis Mwamunyange kwenye  moja ya switch inayotumika kuwasha Pampu na kusukuma maji kutoka  Kibamba itakayopeleka maji kwenye tanki la Kisarawe.
Mafundi wakiendelea na kazi ya matengenezo katika mabomba yanayopeleka maji Tanki la Kisarawe

Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii
WANANCHI wa Kisarawe wanatarajia kuanza kutumia maji safi salama hapo kesho baada ya mradi wa Maji wa Kisarawe kukamilika kwa asilimia 99 kufikia leo. 

Mradi wa Kisarawe wenye thamani ya Bilion 10.6 ulianza kujengwa Juni 2018 baada ya agizo la Rais Dkt John Pombe Magufuli wakati wa kuzindua mtambo wa Ruvu Juu na kuwataka DAWASA kuhakikisha Kisarawe wanapata maji safi na salama.

Agizo hilo limeweza kutekelezwa kwa muda wa mwaka kwa kutumia fedha za ndani za Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam DAWASA.

Hayo yamesemwa leo na Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira DAWASA Jenerali mstaafu Davis Mwamunyange alipotembelea na kukagua mradi huo uliopo kwenye hatua za mwisho kukamilika.

Amesema, kazi kubwa imeshafanyika na palipobaki ni kidogo sana ila kuanzia kesho wananchi na wakazi wa Kisarawe wataanza kutumia maji safi na salama na kuepukana na maradhi yanayosababisha na maji yasiyo salama.

"Tumetekeleza ahadi ya Rais, kama alivyotuagiza na sisi tumeleta mradi huu hapa Kisarawe na wananchi waendelee kuleta maombi ya maji ili waweze kuunganishiwa,"amesema Mwamunyange.

" Kuna marekebisho kidogo katika mabomba yetu, ila hiyo ni kazi ndogo na mafundi wapo kazini wanaendelea na kazi ya kuhakikisha wanaimaliza haraka," amesema

Kwa upande wa Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Mhandisi Cyprian Luhemeja amesema ana furaha kubwa sana kwa kuweza kuukamilisha mradi wa maji wa Kisarawe tena kwa fedha za ndani.

Luhemeja amesema, tayari wameshapokea maombi 1200 kutoka kwa wakazi wa Kisarawe kwa ajili ya kuunganishiwa maji ila malengo ni kupita idadi hiyo ya wateja.

Aidha, amesema wakazi 25,000 watafaidika na mradi huo na anawakaribisha wawekezaji kwenda kuwekeza Wilaya ya Kisarawe kwani huduma ya maji safi na salama ipo na inayotoshelezw.

Mradi huo wa Mkuranga unahusisha ujenzi wa Kituo cha kusukuma maji, kulaza mabomba kwa urefu wa Kilomita 350 kutoka Kibamba hadi Kisarawe pamoja na kujenga tanki la maji lenye uwezo wa kuhifadhia maji Lita Miliomln sita kwa siku.