Leo November 20, 2019 Gumzo linaloendelea hivi sasa ni kuhusu kifo cha Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Afrika Kusini Addelaid Ferreira Watt (51).
Kama inavyoelezwa kwamba kifo hakina taarifa, basi kwa mujibu wa mitandao mbalimbali Afrika Kusini imeripoti kuhusu kifo cha Ferreira Watt aliefariki Duniani kwa kupigwa risasi baada ya bastola ya ushahidi kudondoka katika meza ya Mahakama.
Kwa mujibu wa mitandao huko Afrika Kusini imebainisha kuwa tukio hilo limetokea Novemba 18, 2019 katika Mahakama ya Mkoa Ixopo, Kwazulu-Natal.
Tukio hilo la kustaajabisha limetokea wakati Mwendesha Mashitaka huyo akisimamia kesi ya wizi wa kutumia silaha.
Mkurugenzi wa Mashitaka nchini humo, Elaine Zungu amesema kuwa Ferreira Watt alipigwa risasi katika nyonga akiwa ndani ya chumba cha mahakama akiendesha kesi ya Wizi wa kutumia silaha.
Ameeleza kuwa bastola ilidondoka yenyewe kutoka katika Meza ya mahakama kisha ikafyatuka na risasi zikatoka na kumjeruhi Mwendesha Mashitaka huyo Ferreira Watt katika nyonga.
Inaelezwa kuwa Bastola hiyo ilikuwa ni kielelezo cha ushahidi katika kesi ya Wizi wa Unyanganyi kwa kutumia silaha.
Baada ya kutokea kwa tukio hilo, Ferreira Watt alichukuliwa na kukimbizwa Hospitali ambapo madaktari wakathibitisha kwamba amejeruhiwa katika Nyonga ya Upande wa Kushoto.
Hata hivyo baadaye, ikatolewa taarifa nyingine siku hiyo ya Jumatatu, Novemba 18, 2019 kwamba mwendesha mashitaka huyo amefariki Dunia.