DROO ya makundi ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika pamoja na hatua ya mtoano ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, inatarajiwa kufanyika keshokutwa Jumatano huku Kocha Mkuu wa Yanga, Mkongomani, Mwinyi Zahera akitamba hana hofu na yupo tayari kukutana na timu yoyote wakiwemo Waarab.Droo hiyo inatarajiwa kupangwa jijini Cairo, Misri na Yanga inashiriki Kombe la Shirikisho baada ya kuondolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na Zesco United ya Zambia.Siku hiyo Yanga itamfahamu mpinzani wake watakayekutana naye katika mchezo wa kusaka nafasi ya kufuzu hatua ya makundi ya michuano hiyo na kwa mujibu wa ratiba ya Caf, mchezo wa kwanza utapigwa Oktoba 27, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na marudiano ni Novemba 3, ugenini.Zahera alisema kuwa soka la Afrika limebadilika hivi sasa, kwani viwango vya wachezaji vinafanana hali inayompa matumaini. Alisema amejifunza vitu vingi kuondolewa kwao kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, hivyo amepanga kurekebisha makosa waliyoyafanya ili yasijitokeze katika shirikisho.“Soka la Afrika hivi sasa limebadilika kwa kiwango kikubwa, awali timu nyingi zilikuwa zinazihofia timu za Waarab, lakini hivi sasa hawaziogopi kutokana na ubora wao kupungua. Hivyo, mimi kama kocha nipo tayari kukutana na timu yoyote kutoka Uarabuni, na nina uhakika wa kupata matokeo mazuri nyumbani na ugenini,” alisema Zahera.Miongoni mwa timu ambazo Yanga inaweza kupangwa nazo ni Paradou AC (Algeria), ESAE (Benin), DC Motema Pembe (DRC) na FC San Pedro (Ivory Coast).

Nyingine ni Pyramids (Misri), Bandari (Kenya), Bidvest Wits (Afrika Kusini), TS Galaxy (Afrika Kusini), Proline (Uganda) na Triangle United (Zimbabwe).