KUAPISHWA RASMI KWA MFALME MPYA WA JAPAN 

Dodoma, 19 Oktoba 2019.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt. (Mst) George Mkuchika (Mb.) atahudhuria sherehe za kuapishwa na kutambulishwa kwenye Jumuiya ya Kimataifa kwa Mfalme Naruhito wa Japan zitakazofanyika jijini Tokyo tarehe 22 Oktoba 2019.

Mhe. Mkuchika anamwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ambaye aliakwa katika sherehe hizo na Waziri Mkuu wa Japan, Mhe. Shinzo Abe.

Kwa mujibu wa katiba na sheria za Kifalme za Japan, Mfalme Naruhito amerithi kiti cha Baba yake, Mfalme Akihito ambaye alitangaza kujiuzulu rasmi nafasi yake tarehe 30 Aprili 2019 kutokana na umri wake kuwa mkubwa sanjari na kusumbuliwa na matatizo ya kiafya. Mfalme Naruhito alichukua madaraka hayo tarehe 1 Mei 2019.

Mhe. Mkuchika na ujumbe wake wanatarajia kuondoka nchini tarehe 19 Oktoba 2019 na kurejea tarehe 24 Oktoba 2019.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,