Waziri wa Madini Doto Biteko, ameitaka kampuni ya Mantra Tanzania kuipa nafasi ofisi yake ili kuweza kujiridhisha endapo maombi ya kusitisha kuanza kwa shughuli za uchimbaji wa madini hayo una tija kwa kampuni na Taifa.

Waziri Biteko ametoa kauli hiyo wakati wa kikao baina ya Wizara na uongozi wa Kampuni hiyo ulioitaka wizara kuridhia ombi la kusogeza mbele shughuli za uzalishaji wa madini hayo kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia 2020 mpaka 2024.

Akizungumza hoja hiyo iliyowasilishwa katika kikao hicho, Waziri Biteko alihoji uhakika bei ya madini hayo ifikapo mwaka 2024 katika soko la dunia la endapo utakuwa wakuridhisha na kuwataka kuwasilisha data zao ili ofisi yake iweze kuzifanyia kazi.

“Ni kiashira gani kinachowaonesha kuwa ifikapo 2024 kutakuwa na ongezeko la thamani kwa madini ya urani?” Biteko alihoji.
Aidha, Biteko aliutaka uongozi wa Kampuni hiyo kuwasilisha mchanganuo unaoonesha ongezeko la thamani ya madini ya urani ifikapo 2024 ili wataalamu wa wizara wafanyie kazi na kuishauri wizara juu ya kuridhia au kutoridhia maombi hayo.

Akizungumzia juu ya maamuzi yaliyofikiwa na kampuni hiyo, Rais wa Kampuni ya Mantra Tanzania, Vasiliy Konstantinov alisema bei ya kuuza madini hayo  kwenye soko la dunia imeshuka jambo ambalo litapelekea kampuni na serikali kutokunufaika na uwekezaji huo kutokana na kuwekeza kwa hasara.
Konstantinov alisema kuwa kampuni imeamua kufika na kukaa na wizara ili kupata msaada na kuhakikishiwa uhakika wa kuendelea na uwekezaji huo mara baada ya thamani ya madini hayo kuongezeka ili kuwawezesha kuwekeza kwa faida.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa leseni na Tehama kutoka Tume ya Madini, Yahya Samamba alihoji uamuzi wa Kampuni hiyo kuendelea na uwekezaji ifikapo 2024 endapo hakutokuwa na mabadiliko ya kuridhisha katika soko la dunia. 

Akijibu hoja hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Mantra Tanzania, Alexander Ryabchenko alisema kwa sasa kampuni hiyo iko katika utafiti wa kutafuta njia rahisi isiyotumia gharama kubwa za uwekezaji ili kuifanya kampuni hiyo kuendelea na uzalishaji mara baada ya muda huo kufika hata kama bei ya madini hiyo haitabadilika. 

Mantra Tanzania ni kampuni ya uchimbaji mkubwa wa Madini nchini iliyotolewa na Wizara ya Madini mwaka 2013.
 Waziri wa Madini, Doto Biteko akiwakaribisha wajumbe kutoka Kampuni ya Mantra Tanzania na wataalamu wa Wizara katika kikao kilichojadili juu ya uchimbaji wa madini ya uranium nchini.
 Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango, Augustine Ollal akihoji jambo wakati wa kikao baina ya wizara na Kampuni ya Mantra Tanzania kilichofanyika katika Ofisi ya Waziri wa Madini Doto Biteko (katikati).
 Mkurugenzi Mtendaji wa Mantra nchini Frederick Kibodya akizungumza jambo wakati wa kikao baina ya kampuni hiyo na wizara kilichoongozwa na Waziri wa Madini Doto Biteko.
 Waziri wa Madini, Doto Biteko akimsikiliza kwa makini Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Uranium One Alexander Ryabchenko akizungumza jambo wakati wa kikao baina ya wizara na kampuni hiyo.
 Waziri wa Madini, Doto Biteko na wajumbe walioshiriki kikao baina ya wizara na kampuni ya Mantra Tanzania wakifurahia jambo wakati kikao hicho kikiendelea.
 Waziri wa Madini, Doto Biteko akizungumza kwa simu  na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Nchini(Jina halikupatikana) kuomba nafasi kwa ajili ya uongozi wa kampuni ya Mantra Tanzania kufanya naye mazungumzo kuhusu masuala yanayosimamiwa na mamlaka hiyo.
 Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mantra Tanzania Alexander Ryabchenko akizungumza jambo wakati wa kikao baina ya Wizara na kampuni hiyo.
 Waziri wa Madini, Doto Biteko akiagana kwa kushikana mkono na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Uranium One Alexander Ryabchenko mara baada ya kumaliza kikao baina ya wizara na kampuni hiyo. Katikati ni Rais wa kampuni hiyo Vasiliy Konstantinov
Waziri wa Madini Doto Biteko akizungumza jambo na Rais wa kampuni ya Uranium One Vasiliy Konstantinov.