Na Happiness Shayo, Mwanza
Serikali imewataka watendaji katika taasisi za umma nchini kutenda haki wanapowahudumia watumishi wa umma ili kupunguza mlundikano wa rufaa na malalamiko ya watumishi wa umma yanayowasilishwa Tume ya Utumishi wa Umma dhidi ya waajiri.

Wito huo umetolewa jijini Mwanza na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) wakati wa kikao kazi chake na Watendaji wa Serikali mkoani Mwanza kilichofanyika katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.

“Serikali inaamini katika haki na Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli anataka haki itendeke hususani kwa wanyonge, hivyo mtendaji yeyote atakaebainika kumuonea mtumishi kwa kumnyima stahiki yake ni wazi kuwa serikali itamchukulia hatua za kinidhamu” Dkt. Mwanjelwa amesema.
Dkt. Mwanjelwa amefafanua kuwa, Tume ya Utumishi wa Umma imekuwa ikipokea malalamiko mengidhidi ya watendaji kuwaonea  watumishi wa umma na kuwataka watendaji hao kuwajibika ipasavyo katika nafasi zao ili kuepukana na malalamiko yasiyo ya lazima.

Aidha, Dkt. Mwanjelwa amewaasa watendaji haokutumia muda wao kuwaelimisha watumishi kuhusu Kanuni, Sheria, Taratibu,Nyaraka na miongozo ya kiutumishi iliyopo ili watumishi wapate uelewa wa kutosha kuhusiana na stahiki za kiutumishi wanazostahili kupata.
“Mtumishi anapokuja ofisini kwako tumia muda wako kumuelewesha mtumishi huyo juu ya suala lake, kwa sababu ni sehemu yako ya kazi” Dkt. Mwanjelwa amesisitiza

Akizungumzia kuhusu malalamiko ya watumishi kutobadilishiwa kazi(recategorization) baada ya kujiendeleza, Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. Nyakimura Muhoji amewataka Watendaji hao kuwashauri watumishi walio chini yao kujiendeleza kitaaluma katika kada zao walizopatia ajira(first appointment).

Bw. Muhoji ametoa wito kwa waajiri nchinikuwaingiza watumishi katika mpango wa mafunzo na kuwataka kuwapa ushirikiano wa kutosha watumishi wanaotaka kujiendeleza wenyewe kupitia vyanzo vyao vya mapato, kwani kwa kufanya hivyo watakuwa wametoa fursa kwa watumishi hao kujijengea uwezo kiutendaji” Bw. Muhoji amesema.

Naye, Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilemela, Bw.Said Raphael Kitinga akizungumza kwa niaba ya washiriki wa kikao kazi hicho, ameishukuru serikali kwa elimu ya masuala ya kiutumishi waliyoipata kupitia mada zilizowasilishwa.
Bw. Kitinga ameongeza kuwa, kupitia kikao kazi hicho Watendaji wa Serikali mkoani Mwanza kwa kiasi kikubwa wametatuliwa changamoto zao kiutumishi zilizokuwa zikiwakabili katika maeneo yao ya kazi.

“Tumepata fursa za kutatua matatizo yetu kutokana na ufafanuzi wa masuala mbalimbali ya kiutumishi uliofanyika ’’ Bw. Kitinga amesema.
Kikao kazi hicho kimehudhuriwa na Wakuu wa Wilaya, Watendaji wa Serikali Kuu, Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, Wakala za Serikali, Makatibu Tawala wa Wilaya, Watendaji wa Taasisi za Umma na Wakuu wa Sehemu/Vitengo kutoka Mkoa wa Mwanza lengo likiwa ni kubaini changamoto zinazowakabili, kusikiliza kero zilizopo na kuzipatia ufumbuzi ili kuboresha mazingira ya utendaji kazi kwa watumishi hao.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akizungumza na Watendaji wa Mkoa wa Mwanza (hawapo pichani) wakati wa kikao kazi kilichofanyika jijini Mwanza.

Baadhi ya Watendaji kutoka Mkoa wa Mwanza wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza wakati wa kikao kazi kilichofanyika jijini Mwanza.

Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. Nyakimura Muhoji akijibu hoja wakati wa kikao kazi kati ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb), Makamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma na Watendaji wa Mkoa wa Mwanza kilichofanyika jijini Mwanza.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) (kulia) akiteta jambo na Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma Mhe.John Haule wakati wa kikao kazi kati yake na Watendaji wa Mkoa wa Mwanza kilichofanyika jijini Mwanza. Kushoto ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilemela Bw. Said Raphael Kitinga.