Ujenzi wa Machinjio Vingunguti Usiku na Mchana, Wamvuta Waziri
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ametembelea mradi wa ujenzi wa machinjio ya Vingunguti na kuvutiwa na kasi ya ujenzi wa mradi huo inayofanywa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ambapo amelitaka shirika hilo kuhakikisha linajenga jengo lenye ubora.

Akiwa katika ziara yake ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo jana, Dkt. Mabula alisema pamoja na mradi huo kutakiwa kukamilika katika kipindi cha miezi mitatu badala ya 12 ya awali lakini hatarajii kuona Shirika la Nyumba linajenga jengo lililo chini ya kiwango.

Amesema NHC ni shirika la umma lenye kila fani katika masuala ya ujenzi hivyo basi ujenzi wa mradi huo ujenge imani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na watanzania kwa kukamalisha katika kipindi cha miezi mitatu.

Dkt Mabula amesema, maelezo ya Rais kuhusiana na mradi wa machinjio ya Vingunguti ubadilishe fikra za Shirika la Nyumba la Taifa katika miradi yake mbalimbali sambamba na kuonesha uwezo katika miradi waliyopewa kwa kujenga kwa kasi na kwa muda mfupi ukilinganisha na makampuni mengine ya ujenzi

‘’Tuondoke katika fikra tuliyokuwa nayo huko nyuma, tujenge trust kwa mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania’’ amesema Dkt Mabula

Kwa upande wake Meneja Mawasiliano wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Muungano Saguya alimueleza Naibu Waziri kuwa shirika hilo limejipanga kufanya kazi usiku na mchana kuhakikisha linakamilisha ujenzi katika muda uliopangwa

Alisema ujenzi wa mradi huo wa machinjio ya Vingunguti umefikia hatua nzuri na ana imani kutokana na jinsi shirika lilivyojipanga katika mradi huo, ujenzi wake utakamilika katika muda uliopangwa kama ilivyoelekezwa na Rais.