Kampuni ya TBL imeendelea kung’ara baada ya kuibuka mshindi wa kwanza katika sekta ya viwanda vya vinywaji kwenye  tuzo ya Rais ya Mzalishaji bora iliyofanyika katika hoteli ya Serena, jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.

Mgeni rasmi katika hafla hiyo ambayo hutayarishwa na Shirikisho la wenye Viwanda nchini (CTI), alikuwa ni Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa.

Mbali na kuibuka mshindi wa kwanza katika sekta ya viwanda vya vinywaji, TBL pia iliibuka mshindi wa pili katika sekta ya viwanda.

Akiongea kuhusu ushindi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa TBL Group, Philip Redman alisema “TBL tumejipanga kuendesha viwanda nchini Tanzania kwendana na viwango vya kimataifa, ushindi huu unadhihirisha dhamira yetu hiyo na ndio maana pia viwanda vyetu vinashikiria rekodi ya kuwa miongoni mwa viwanda bora duniani”.

Redman, alisema kuwa TBL ni mdau mkubwa wa kuunga jitihada za Serikali za kuifanya Tanzania nchi ya viwanda sambamba na kufanya uwekezaji unaochagia kukuza shughuli za kijamii na uchumi wa nchi.

“Mpango wetu wa kununua malighafi kwa asilimia 70% nchini kama vile Shahiri,mtama na mahindi utafanikisha kuinua maisha maisha ya wananchi kwa haraka sambamba na kufikia uchumi wa kati hadi ifikapo mwaka 2025”, alisema.


TBL pia ni kampuni ambayo imekuwa ikiendesha biashara zake kwa kuzingatia taratibu za nchi na inafanya kazi na wadau mbalimbali sambamba na kutoa kipaumbele cha kutumia malighafi za ndani kwa ajili ya kutengenezea chapa mbalimbali za bia ambazo zinakubalika kwa kiasi kikubwa  kwa wateja katika masoko ya ndani.

Ikiwa uwezekaji wake umewezesha kuchagia zaidi ya shilingi bilioni 500 za mapato ya Serikali kupitia kukusanya na kulipa kodi na kufanikisha miradi ya kusaidia jamii,TBL pia imekuwa mstari wa mbele kuwekeza katika teknolojia za kisasa,wafanyakazi wake na wadau wake inaoshirikiana nao katika biashara.