Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu, akionesha moja ya bango lenye maelezo ya jinsi ya kijikinga na ugonjwa wa Ebola mbele ya Waandishi wa Habari (Hawapo pichani), katika Mkutano uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Julias Nyerere Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe.Ummy Mwalimu, akisisitiza jambo kwa Waandishi wa Habari (hawapo pichani), kuhusu uvumi wa ugonjwa wa Ebola, katika Mkutano uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Julias Nyerere Jijini Dar es Salaam leo Oktoba 3, 2019.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe.Ummy Mwalimu, akifafanua jambo kwa Waandishi wa Habari (hawapo pichani), kuhusu uvumi wa ugonjwa wa Ebola, katika Mkutano uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Julias Nyerere Jijini Dar es Salaam leo Oktoba 3, 2019.
Mkurugenzi wa Huduma za Kinga Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt.Leonard Subi akiandika anayoyasikia kwenye Mkutano wa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe.Ummy Mwalimu(kushoto) wakati wa mkutano wake na Waandishi wa Habari uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Julias Nyerere Jijini Dar es Salaam leo Oktoba 3, 2019. (Picha na Idara ya Habari-MAELEZO).

Mwenendo wa Ugonjwa wa Ebola unaoendelea kuripotiwa nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC)

Wizara imekuwa ikifuatilia kwa karibu mwenendo wa ugonjwa wa Ebola unaoendelea kuripotiwa nchini DRC na kuchukua hatua za tahadhari za kuzuia na kukabiliana na ugonjwa huu hususani kwa kuwa kwa sasa ugonjwa huu unaendelea kusambaa na kuingia kusini mwa DRC. Takwimu zinaonyesha kuwa hadi kufikia tarehe 30 Septemba 2019, jumla ya wagonjwa 3,194 walithibitishwa kuwa na ugonjwa huu, na vifo 2133 (CFR 66.8%). Kutokana na ukaribu wa nchi hii na Tanzania, Wizara imeendelea kuchukua hatua za utayari kuzuia na kujiandaa kukabiliana na ugonjwa huu

Hatua za utayari na kujiandaa kukabiliana na ugonjwa huu nchini ni pamoja na kuimarisha uchunguzi wa Wasafiri kwenye mipaka yetu yote. Kuimarisha utambuzi katika ngazi ya vituo vya kutolea huduma za Afya; Kuhakikisha uwepo vya Vifaa Kinga hususani kwa watumishi wa Afya; Kuimarisha utambuzi wa Ugonjwa na kuendelea kutoa Elimu kwa wananchi kuhusu namna ya kujikinga ugonjwa huu. Wizara inayo namba ambayo hutumika bila malipo na wananchi kutoa taarifa za kuwepo kwa tetesi za ugonjwa huu ambazo ni 0800110124 au 0800110125.

Kuanzia 2018 hadi sasa, tetesi 28 za wagonjwa wanaohisiwa kuwa na Ebola (washukiwa 2 kwa mwezi Septemba), zimekwisha kutolewa taarifa na uchunguzi kufanyika kwa ukamilifu na kuthibitisha wagonjwa hawa hawakuwa na Ebola, na taarifa zake kupelekwa pia katika Shirika la Afya Duniani. Aidha Wizara imeendelea kufanya pia mazoezi ya kujinoa na kijipima utayari wa kukabiliana na ugonjwa huu (Simulation Exercises) katika mikoa ya Dar es Salaam, Kagera, Kigoma, Kilimanjaro na Arusha.

NAPENDA KUSISITIZA KUWA HADI SASA HAKUNA MGONJWA ALIYETHIBITISHWA KUWA NA UGONJWA WA EBOLA HAPA NCHINI. WIZARA INAWASIHI WANANCHI KUTOKUWA NA HOFU NA KUPUUZA TAARIFA ZINAZOTOLEWA KILA KUKICHA NA BAADHI YA VYOMBO VYA HABARI NA MITANDAO YA KIJAMII.

Ndugu Wanahabari,

Katika kudhibiti ugonjwa wa Ebola na magonjwa mengine ya milipuko yenye madhara makubwa duniani, nchi yetu kila wakati imekuwa mstari wa mbele ikiwa ni pamoja na kusimamia kwa ukamilifu na kutekeleza Kanuni za Kimataifa za Afya (International Health Regulation - IHR 2005).

Mnamo mwaka 2016, Tanzania ilikuwa nchi ya kwanza duniani kuweza kukubali bila kipingamizi kuleta wataalam duniani kuja kupima utayari wa nchi yetu katika kukabiliana na magonjwa haya hatarishi (Joint external evaluation). Hatua hii kubwa na ya uwazi ilifanywa kwa mara ya kwanza Duniani, kama moja ya njia ya kuhakikisha nchi wanachama wa Shirika la Afya Duniani, wanatekeleza Kanuni hizi za Kimataifa (IHR 2005).

Aidha nchi nyingine zenye uwezo mkubwa duniani zilisita kufanyiwa tathmini hadi miaka miwili baadae, na nyingine hadi sasa hazijafanya zoezi hili. Hivyo basi, taarifa zinazoenea kuelezea kuhusu Tanzania kutokuweka wazi taarifa za magonjwa hususan uwepo wa ugonjwa wa Ebola nchini, si za kweli na hivyo ziendelee kupuuzwa.

Taratibu za utoaji wa taarifa za magonjwa ya milipuko zinajulikana na ninatoa rai kwa sote tuzingatie sheria na taratibu za nchi husika na za kimataifa.

Ikumbukwe kuwa, ugonjwa wa Ebola ambao unaweza kusambaa kwa haraka, na ambao madhara yake ni makubwa na yanajulikana duniani kote, kamwe hauwezi kufichwa na nchi yetu. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua madhara makubwa ya kuficha ugonjwa kama huu kwa wananchi.

Narudia tena na kuwataka wananchi kutulia na kupuuza taarifa zisizo rasmi kutoka kwenye baadhi ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, maana HAKUNA UGONJWA WA EBOLA NCHINI TANZANIA. Inaonekana kuna njama ovu za kueneza taarifa hasi dhidi ya nchi yetu. Ninaendelea kuwasihi Wananchi kuwa watulivu na kushikamana kwa pamoja katika kuzuia ugonjwa huu usiiingie nchini.

Aidha, Serikali inapenda kuwahakikishia Mataifa yote kuwa nchi yetu ni SALAMA na HATUNA UGONJWA WA EBOLA. Nirudie tena kusisitiza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na nchi na mashirika mbalimbali ya kimataifa ikiwemo Shirika la Afya Duniani katika kujenga utayari wa kukabiliana na tishio la ugonjwa wa Ebola.

Na endapo kutatokea mtu atakaethibishwa kuwa na ugonjwa wa Ebola nchini tutaendelea kuzingatia miongozo na taratibu za kimataifa ikiwemo kutoa Taarifa WHO kwa mujibu wa Kanuni za Kimataifa za udhibiti wa magonjwa hatari ya kuambukiza (IHR 2005).

Kipaumbele cha Wizara kwa sasa ni kuendelea kuimarisha utayari wa kukabiliana na ugonjwa huu usiingie nchini na endapo kutatokea kisa cha ugonjwa huu nchini tuweze kukabiliana nao na kuudhibiti mara moja.