Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akimkaribisha Balozi wa Sweden nchini Tanzania, Mhe. Anders Sjoberg alipotembelea Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) Kampasi ya Dar es Salaam jana kwa lengo la kubadilishana uzoefu kuhusu masuala ya Utumishi wa Umma kwa nchi za Sweden na Tanzania.
 Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) na Balozi wa Sweden nchini Tanzania, Mhe. Anders Sjoberg wakishuhudia jinsi mashine ya kupiga chapa inavyofanya kazi mara baada ya Balozi kutembelea Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC)  jana kwa lengo la kubadilishana uzoefu kuhusu masuala ya Utumishi wa Umma kwa nchi za Sweden na Tanzania. Wa kwanza kulia ni Mtendaji Mkuu na Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Dkt. Emmanuel Shindika
 Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) na Balozi wa Sweden nchini Tanzania, Mhe. Anders Sjoberg wakionyesha zawadi ya ramani ya Afrika yenye nembo ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania baada ya Balozi huyo kukabidhiwa zawadi hiyo na Naibu Waziri kuonyesha ushirikiano mwema baina ya Tanzania na Sweden katika masuala ya utumishi wa umma wakati Balozi aliotembelea chuoni hapo jana kwa lengo la kubadilishana uzoefu kuhusu masuala ya Utumishi wa Umma kwa nchi za Sweden na Tanzania.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) na Balozi wa Sweden nchini Tanzania, Mhe. Anders Sjoberg wakicheza wimbo unaosifu utendaji kazi wa Marais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuanzia Awamu ya Kwanza mpaka sasa wa kwaya ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania  wakati Balozi aliotembelea chuoni hapo jana kwa lengo la kubadilishana uzoefu kuhusu masuala ya Utumishi wa Umma kwa nchi za Sweden na Tanzania. Kushoto kwa Balozi ni Kaimu Katibu Mkuu Utumishi, Bw. Mick Kiliba.

Na Mary Mwakapenda, Dar es Salaam

Serikali ya Sweden imeipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Rais, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuongoza nchi ikizingatia utawala bora hususani katika mapambano dhidi ya rushwa.
Pongezi hizo zimetolewa na Balozi wa Sweden nchini Tanzania, Mhe. Anders Sjobers alipokuwa akiwasilisha mada kuhusu uzoefu wa nchi yake katika masuala ya utumishi wa umma kwa wanafunzi na watumishi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) Kampasi ya Dar es Salaam.

Balozi Sjobers amesema, katika nchi yao tatizo la rushwa halipo kabisa kwani Serikali iliongoza vema mapambano dhidi ya rushwa, hivyo ameipongeza Serikali ya Awamu ya Tano ya Tanzania inavyoendesha vizuri mapambano dhidi ya rushwa kwa ajili ya maslahi ya umma na maendeleo ya taifa kwa ujumla.

Katika mada yake, Mhe. Balozi amefafanua kuwa, nchini Sweden suala la Watumishi wa Umma kuwajibika kwa wananchi limepewa kipaumbele kwani wananchi wote wanahitaji huduma sawa bila ubaguzi wa aina yoyote.
Kwa upande wake, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mary Mwanjelwa (Mb) 
ameishukuru Serikali ya Sweden kwa kutambua juhudi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano kwenye eneo la utawala bora.

“Tunaishukuru Serikali ya Sweden kwa kutambua jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano kuimarisha utawala bora nchini hasa katika mapambano dhidi ya rushwa,” Mhe. Dkt. Mwanjelwa amesema.
Aidha, katika eneo la uwajibikaji, Mhe. Mwanjelwa ametumia fursa hiyo kuwasisitiza  Watumishi wa Umma nchini kuwahudumia wananchi vizuri na kwa wakati kama Serikali inavyosisitiza kila mara.

“Ukiwa Mtumishi wa Umma, tambua wazi kuwa wewe ndio injini kwani wananchi wanahitaji huduma bora kutoka kwako, hivyo unatakiwa muda wote kuwahudumia wananchi kwa uadilifu na bila ubaguzi wa aina yoyote,” Mhe. Dkt. Mwanjelwa amesisitiza.
Kuhusu uhusiano uliopo kati ya Sweden na Tanzania, Mhe, Mwanjelwa amesema Nchi hizo mbili zimekuwa na uhusiano mzuri tangu utawala wa Serikali ya Awamu ya Kwanza na uhusiano huo umeendelea kushamiri hadi sasa kwenye utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano.

“Uhusiano kati ya Sweden na Tanzania umeanza tangu mwaka 1970 walipojenga Chuo cha Utumishi wa Umma Tawi la Tabora kwa asilimia 80 na bado tumeendelea kuwa na uhusiano mzuri,” Mhe. Dkt. Mwanjelwa ameongeza. 
Mhe. Balozi Sjoberg alitembelea Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC)  jana kwa lengo la kubadilishana uzoefu kuhusu masuala ya Utumishi wa Umma kwa nchi za Sweden na Tanzania na kesho atatembelea Chuo cha Utumishi wa Umma, Tawi la Tabora ili kuona chuo hicho kilichojengwa na Serikali yao na kuangalia jinsi watakavyokienzi.