Msanii wa filamu, mjasiriamali na mbunifu wa mavazi Jacqueline Wolper,  ameweka wazi kuwa  hana tofauti yoyote na msanii mwenzake Wema Sepetu pamoja na kufunguka 'issue' za kuringa.


Jacqueline Wolper alizua maswali mengi mara baada ya kutokea kwenye 'Birthday Party' ya Wema Sepetu, iliyofanyika wiki iliyopita, ambapo wawili hao wanadaiwa walikuwa na bifu siku za nyuma.

Alipodakwa na kamera za EATV & EA Radio Digital,  ametaja sababu zilizomfanya ahudhurie kwenye 'Birthday' hiyo hali ya kuwa watu wanajua wana tofauti.

"Mimi nipo tofauti sana, sinaga kinyongo na mtu halafu napenda sana watu na napenda ku-support, ikitokea kama nina nafasi kuna sehemu nimealikwa nitakwenda , watu waache kufuatilia habari za kuandikwa inatakiwa waamini Wolper hana bifu na mtu yeyote, pia namshukuru Mungu nimekuwa mkweli kama nina tofauti na mtu huwa nasema siwezi kuficha hisia zangu", alisema Wolper.

Akizungumzia suala la kuringa, Wolper amesema kuwa watu walichelewa kumuelewa na yeye huwa haringi kabisa ila kujitenga kwake na kuwa bize  ndiyo kunafanya watu wamuone hivyo.