Serikali imeshauriwa kupitia upya sheria za vilevi, ikiwemo kuweka masharti kwa matangazo ya uzalishaji, uhamasishaji, uuzaji na udhamini wake na kuonyesha onyo la athari zake kwa watumiaji sambamba na kudhibiti pombe za kienyeji ambazo hutengenezwa chini ya viwango.

Mwenyekiti wa Tanzania Public Health Association (TPHA), Dkt. Mashombo Mkamba ametoa ushauri huo jijini Dodoma jana, katika maadhimisho ya mtandao wa wadau unaopambana na unywaji wa pombe kupita kiasi (TAAnet).

Amesema kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya mwaka 2016, zaidi ya watu milioni tatu duniani hufariki kutokana na matumizi ya pombe, ambapo zaidi ya robo tatu ya vifo hivyo ni wanaume pekee.

“Matumizi ya pombe na athari zake ni tatizo linalozidi kukua nchini, na linahitaji kudhibitiwa haraka iwezekanavyo ili kuzuia ongezeko la unywaji pombe katika jamii, maana hali si shwari kwa baadhi ya maeneo hasa zile za kienyeji maana unywaji wake na mazingira ya uandaaji si rafiki,” ameongeza Mkamba.

Aidha amesema matumizi ya pombe kupita kiasi husababisha zaidi ya asilimia tano ya mzigo wa magonjwa duniani, kwa takwimu za Shirika la Afya Duniani  (WHO) katika ripoti yake ya hali ya dunia juu ya unywaji pombe na afya iliyotolewa mwaka 2018.

Mkamba amefafanua kuwa katika taarifa hiyo, WHO imependekeza uwepo uwezo na ujuzi wa kisayansi kwa watunga sera juu ya ufanisi wa mikakati iliyowekwa, ili kuzuia madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na matumizi ya pombe yaliyokithiri.

“WHO inapendekeza watunga sera wanapaswa kutilia mkazo katika udhibiti uuzaji wa vinywaji holela, na kusimamia upatikanaji holela wa pombe, kufanya maboresho ya sheria ya usalama barabarani ikiwamo kutengeneza sera ili kudhibiti madereva wanaoendesha magari wakiwa wamelewa,” ameongeza Mkamba.

Kwa upande wake Katibu wa TAAnet, Bi. Gladness Munuo amesema ujumbe walionao ni kuikumbusha jamii madhara ya unywaji pombe uliopitiliza.

“Endapo kutakuwa na sera ya udhibiti wa matumizi mabaya ya pombe, jamii wadau wa vileo hasa wanaume wataacha unywaji uliopitiliza na kuepuka athari za kiafya zinazoweza kuwapata na kupunuza nguvukazi ya Taifa,” amesema Bi. Munuo.