Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Uchambuzi na Ushauri wa Kazi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Nolasco Kipanda akifunga mafunzo ya wadau yenye lengo la kuwajengea uwezo wa Ufuatiliaji na Tathmini watendaji wa Serikali yaliyofanyika jijini Dodoma.
 Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya wadau yenye lengo la kuwajengea uwezo wa Ufuatiliaji na Tathmini watendaji wa Serikali wakifuatilia mada wakati wa mafunzo hayo jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa Idara ya Mikataba ya Utendaji Kazi Serikalini, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Hassan Kitenge akiwasilisha mada wakati wa mafunzo ya wadau yenye lengo la kuwajengea uwezo wa Ufuatiliaji na Tathmini watendaji wa Serikali yaliyofanyika jijini Dodoma.

Na Happiness Shayo – Dodoma
Serikali kwa kushirikiana na Asasi Zisizo za Kiserikali inatarajia kuboresha mifumo ya Ufuatiliaji na Tathmini ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa za miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali kwa manufaa ya Taifa.

Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Uchambuzi na Ushauri wa Kazi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw.Nolasco Kipanda wakati akifunga mafunzo ya wadau ya siku mbili yenye lengo la kuwajengea uwezo wa Ufuatiliaji na Tathmini watendaji wa Serikali yaliyofanyika jijini Dodoma.

Bw. Kipanda amesema kuwa mifumo ya Ufuatiliaji na Tathmini iliyoko sasa haiwasiliani hivyo kuleta changamoto ya upatikanaji wa taarifa ya pamoja ya utekelezaji wa miradi mbalimbali serikalini.

“Kuna mifumo mingi ya Ufuatiliaji na Tathmini ambayo haiongei, hivyo kwa kushirikiana na AZAKI tunajipanga kuboresha mifumo hiyo ili iweze kuwasiliana na kutoa taarifa ya pamoja inayoweza kutumiwa na wadau wakati wa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Serikali” Bw. Kipanda amesema.

Bw. Kipanda amefafanua kuwa, ili kufikia azma ya kuboresha mifumo hiyo, unahitajika muda wa kutosha, rasilimali fedha, rasilimali watu na mikakati thabiti, hivyo kupitia mafunzo hayo wadau wametoa maoni yatakayowezesha maboresho.

Bw. Kipanda ameongeza kuwa, maoni ya wadau yaliyopatikana katika mafunzo hayo yatawasilishwa kwenye mamlaka nyingine za serikali ili yatumike kuongeza ufanisi wa utendaji kazi.

Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Bi. Esther Ngulwa ambaye ni Afisa Ufuatiliaji na Tathmini wa taasisi ya Aga Khan Foundation East Africa  amesema, ili Serikali ifanikiwe kuboresha mifumo ya Ufuatiliaji na Tathmini ni vema ikawa na mikakati endelevu ya kuwakutanisha wadau wa kada hiyo kwa ajili ya kukusanya maoni kwa lengo la kuisaidia Serikali kuleta maendeleo kwa wananchi.

Bi. Ngulwa ameongeza kuwa, endapo mifumo ya Ufuatiliaji na Tathmini itaunganishwa pamoja itawezesha upatikanaji wa taarifa na kubaini maeneo yenye mapungufu na hatimaye kuangalia namna bora ya kufikia malengo ya Taifa.

Naye, Meneja wa Uchambuzi wa Sera na Bajeti wa taasisi ya Policy Forum Bw. Nicholaus Lekule ameipongeza serikali kwa kuwa na mifumo mizuri ya Ufuatiliaji na Tathmini na kuitaka Serikali kufanyia kazi pendekezo la kuwa na mifumo inayozungumza.

Mafunzo hayo ya siku mbili yameandaliwa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa kushirikiana na “Centre for Learning on Evaluation and Results CLEAR-AA” ya Chuo cha Witwatersrand nchini Afrika Kusini.