KAMPUNI ya Mara nchini Rwanda imezindua simu mbili za kisasa, (smartphones) ikiwa ni nchi ya kwanza ‘kutengeza aina hiyo ya simu barani Afrika’,  hatua inayodhihirisha maono ya nchi hiyo ya kuwa bingwa wa masuala ya teknolojia.
Simu hizo ambazo zimepewa jina Mara X na Mara Z zitatumia mfumo wa Google wa Android na zinatarajiwa kuuzwa kuanzia Dola za Marekani 190 hadi 130 ambayo ni sawa na shilingi zaTanzania 436,850 hadi 298,923.


Simu hizo kwa mujibu wa vyombo vya habari duniani, zinatarajiwa kushindana na simu za kampuni ya Samsung, ambazo simu zake ni za bei nafuu zaidi kwani huanzia dola za Marekani 54 ikiwa ni sawa na shilingi za Tanzania takribani 130,000 huku simu nyingine zisizo na alama zikiuzwa dola 37 sawa na shilingi 85,000.


Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Reuters, Afisa Mkuu Mtendaji wa Kampuni ya Mara, Ashish Thakkar, amesema kwamba bidhaa yao hiyo inawalenga wateja walio tayari kulipa zaidi kwa bidhaa za hali ya juu.
Akizungumzia mtaji wa uwekezaji wa kampuni hiyo, Thakkar amesema kiwanda hicho kimegharimu Dola milioni 24 kujenga na kinaweza kutengeza simu 1,200 kwa siku.


Kwa upande wake, Rais Kagame baada ya kutembelea kiwanda hicho amesema, anatumai kwamba simu za aina hiyo zitaongeza utumizi wa simu aina ya smartphone miongoni mwa raia wa Rwanda ambapo kwa takwimu za hivi karibuni watumiaji wa simu nchini humo ni asilimia 15 tu.