Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ametengua agizo la mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sofia Mjema aliyepiga marufuku ibada kufanyika katikati ya wiki hivi karibuni.

Makonda ametoa kauli hiyo leo baada ya kuulizwa katika mkutano wake na waandishi wa habari baada ya video kusambaa mitandaoni ikimuonyesha mkuu huyo wa wilaya akipiga marufuku.

“Tunajua kwenye kuomba Mungu ni mara tatu yaani  Ijumaa, Jumamosi na Jumapili hizi siku nyingine marufuku nyinyi kazi mnafanya saa ngapi? Mnasema nimemuona mkombozi, unamuonaje bila kufanya kazi. Zunguka, ungezunguka mpaka kiama kama hufanyi kazi hazizunguki hizo.” DC Mjema katika video yake alisema siku nyingine wananchi wa Ilala wanatakiwa kufanya kazi,

“Natengua kauli ya Sofia watu waendelee kwa imani zao bila kuathiri sheria za nchi. Viongozi tunapaswa kuwa makini tunapoingia kwenye masuala ya dini, dini ni imani,” amesema RC Makonda.

“Mimi ni mlokole huwezi kunipangia muda wa kusali. Tuwe na kiasi tunapoongelea imani za watu. Kuhamasisha watu kufanya kazi ni jambo jema ila lisiloingilia misingi ya imani nyingine.”