Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii

Naibu Waziri wa Maji Jumaa Aweso amewahakikishia wanafunzi wa shule ya Sekondari Pugu kuwa watapata maji safi na salama.

Hayo ameyasema baada ya kutembelea shule hiyo ambayo alisoma mchepuo ya SayansI PCB na kuhitimu elimu yake ya kidato cha sita mwaka 2007.

Aweso, amesema kuna mradi wa maji kutoka Kisarawe kwenda Pugu wenye thamani ya Bilion 6 ambapo amewaagiza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira DAWASA kupeleka maji shuleni hapo.

"Nafahamu changamoto ya maji katika shule hii, mimi nimesoma hapa ilifikia kipindi unakaa hadi wiki tatu hujayapata maji, kero ilikuwa kubwa sana," amesema.

"Kuna mradi mkubwa wa maji unaotoka Kisarawe hadi Pugu, nilishawaagiza Dawasa wakati nafanya Mkutano kuwa maji lazima yafike Shule ya Pugu," 

 Aweso amesema, kuna watu mashuhuri, viongozi wamepita hapa Pugu Sekondari na mimi nawaomba wasiache kuja kutembelea hapa na kuhakikisha wanaisaidia kwa namna moja au nyingine.

 "Kuna Viongozi wengi na watu mashuhuri wamepita hapa Pugu Sekondari na mkuu wa Shule usisite kuwaalika kwa ajili ya kuja kuisaidia shule yao na mimi nawahakikishia kuwa ntarudi tena hapa," 

"Mimi nimesoma hapa, hata katibu Mkuu wangu wa Wizara ya Maji Kitila Mkumbo amesoma hapa na kutokana na hilo lazima nihakikishe maji yanafika kwenye shule hii, mwalimu Mkuu usisite kusema lolote kwani wengi tumepita kwenye shule hii," amesema Aweso.

Aweso ametembelea shule hiyo na kusalimiana na wanafunzi wa Mchepuo wa Sayansi PCB, na kuwataka wasome kwa bidii ili waje kuisaidia shule yao hapo baadae.
 Naibu Waziri wa Maji Jumaa Aweso  akiwa amekaa katika meza aliyokuwa anaitumia wakati anasoma shule ya Sekondari Pugu, leo ametembelea shule hiyo na kuwahakikishia wanafunzi wa hapo watapata maji safi na salama.
 Naibu Waziri wa Maji Jumaa Aweso akisalimiana na walimu waliomfundisha wakati anasoma shule ya Sekondari Pugu, leo ametembelea shule hiyo na kuwahakikishia wanafunzi wa hapo watapata maji safi na salama.
Naibu Waziri wa Maji Jumaa Aweso akiwa amepiga picha ha pamoja na wanafunzi na walimu wa Shule ya Sekondari Pugu baada ya kutembelea shule hiyo.