Msanii wa Bongofleva Ommy Dimpoz, amesema hatua ya uzinduzi wa Utoaji Tiba wa kusafisha damu kwa wagonjwa wa Figo (Dialysis), kwenye hospitali ya Lugalo Dar es salaam itasaidia wananchi kutatua tatizo la figo.


Akiongea leo Oktoba 23, 2019 kwenye uzinduzi huo uliofanyika Hospitalini Lugalo. Ommy amesema hatua hizo za kuboresha na kupanua utoaji wa huduma za afya zitapunguza gharama kwa wananchi wa kipato cha chini.

'Hospitali zetu zinajitahidi sana licha ya uchache wa vifaa, kazi bado ni kubwa lakini naamini kwa serikali ya sasa inayomwangalia mwananchi wa chini tutafika mbali na kuepusha sasa wananchi kufuata matibabu nje', amesema Ommy.

Aidha msanii huyo ambaye aliwahi kupata matatizo ya koo na kutibiwa nje ya nchi, ameeleza kuwa hatua ya watalaamu kupelekwa Ujerumani kupata matibabu itasaidia kuboresha matibabu hayo na kwa gharama nafuu.

Mapema leo Waziri wa Ulinzi Hussein Mwinyi amezindua huduma hiyo ya Dialysis, ambapo ameweka wazi kuwa itapunguza msongamano katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.