Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiangalia moja ya Majalada ya Ardhi katika Ofisi za ardhi za jiji la Tanga mwishoni mwa wiki wakati wa ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi mkoani Tanga. Katikati ni Mkuu wa Idara ya Ardhi wa Halmashauri ya Jiji la Tanga Strawton Thobias.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akisalimiana na Mkuu wa Idara ya Ardhi katika halmashauri ya Jiji la Tanga Strawton Thobias mwishoni mwa wiki alipowasili katika jiji hilo wakati wa ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi mkoani Tanga.


Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiangalia moja ya eneo lenye mgogoro lililopo Mtaa wa Independence katikati ya jiji la Tanga wakati wa kutembelea maeneo yenye mgogoro wa ardhi katika jiji hilo mwishoni mwa wiki. Kulia ni Mkuu wa mkoa wa Tanga Martine Shighela na kushoto ni mtoto wa mmiliki wa eneo hilo Paul Charles. 
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiwa katika picha ya pamoja na uongozi na watendaji wa sekta ya ardhi wilaya ya Pangani mkoani Tanga mwishoni mwa wiki wakati wa ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi mkoani Tanga. Kulia kwa Naibu Waziri ni Mkuu wa wilaya ya Pangani Zainab Issa.

Na Munir Shemweta, WANMM TANGA.


Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amemuagiza Mkurugenzi wa Jiji la Tanga Daud Mayeji kupitia viwanja vyote vinavyodaiwa ni mali ya jiji hilo lakini vinamilikiwa na watu wengine.Hata hivyo, wakati Dkt Mabula akitoa agizo hilo eneo maarufu la ufukwe katika jiji la Tanga la Bathing Club lililopo Raskazone Tanga limerejeshwa kwa halmashauri ya jiji la Tanga baada ya mmili wake kulitumia kwa muda mrefu.Eneo hilo la ufukwe ambalo wananchi walikuwa wakienda kwa kulipia limeelezwa kuwa ni moja ya maeneo ambayo nyaraka zake zilikuwa zikioonesha linamilikiwa na Jiji la Tanga lakini lilikuwa chini ya watu wengine.Dkt Mabula aliagiza kupitiwa kiwanja kimoja baada ya kingine na kuwataka wamiliki wake kwenda na nyaraka zinazoonesha umiliki wa maeneo yao kama ni halali na kama ni halali walipataje maana bado yanasomeka kama mali ya jiji la Tanga.


‘’ Ikibainika kuwa wamiliki wake wanamiliki isivyo halali maeneo hayo basi mali hizo zote lazima zirudi serikalini maana kumbukumbu zinaonesha maeneo hayo bado ni mali ya jiji la Tanga’’ alisema Dkt Mabula.


Akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga Martine Shighela wakati wa kutembelea baadhi ya maeneo hayo, Dkt Mabula aliitaka Ofisi ya Halmashauri ya Jiji la Tanga kwenda mtaa kwa mtaa, kuyatambua maeneo husika na kupata nyaraka zinazoonesha umiliki wa maeneo hayo kama ni halali na kama ni halali ifahamu yalipatikanaje wakati hadi sasa kumbukumbu zinaonesha ni mali ya jiji la Tanga.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, agizo hilo ni kwa halmashauri zote hasa katika yale maeneo yaliyotaifishwa na serikali na kuwa mali ya umma lakini bado yanaendelea kumilikiwa na watu wengine huku wengine waliouziwa maeneo wakishindwa kukamilisha malipo yao.

‘’ Kuna baadhi ya maeneo serikali iliwarudishia wenyewe na mengine serikali ilipangisha kama rasilimali zake lakini bado maeneo hayo yanamilikiwa na watu wengine.’’ alisema Naibu Waziri.

Mkurugenzi wa Jiji la Tanga Daud Mayeji alimueleza Naibu Waziri kuwa katika jiji lake kuna maeneo yanaoyoonesha kuwa yanamilikiwa na jiji lakini maeneo hayo bado yanamilikiwa na watu wengine na jiji lake lilifanikiwa kurejeshewa eneo la Bathing Club lililopo Raskazone. Aidha Mayeji alisema jiji lake linakabiliwa na chanagamoto ya baadhi ya maeneo yake kumilikiwa na taasisi za serikali ambazo zimeshindwa kulipa fidia maeneo iliyotwaa kwa wananchi.

Mkurugenzi wa Halamashauri ya Wilaya ya Handeni William Makufwe alitaka kuwekwa kwa gharama halisi za upimaji kwa kuwa hivi sasa kumekuwa na tofauti kubwa ya gharama za upimaji jambo linalowafanya wanapotoa maagizo ya upimaji na kutaka kutolewa muongozo wa gharama za upimaji, upangaji kwa nchi nzima ili kuondoa sintofahamu.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi Gracian Makota ameomba kupatiwa Afisa Ardhi Mteule kwa kuwa anayewahudumia sasa kutoka Korogwe wakati mwingine anashindwa kufanya hivyo kutokana na changamoto au geographia ya wilaya ya Kilindi hasa pale inapotokea miundombinu kuharibika.

Wakati huo huo, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amewajia juu watunza kumbukumbu wa Masijala ya Ardhi katika halmashauri za Jiji la Tanga na ile wilaya ya Pangani mkoani Tanga kwa kushindwa kuzingatia taratibu za utunzaji majalada ya ardhi jambo alilolieleza kuwa linasababisha migogoro ya ardhi.

Akiwa katika ziara yake mkoani Tanga, Dkt Mabula alibaini utunzaji wa kumbukumbu za Majalada ya ardhi usiozingatia taratibu za utunzaji na kuagiza ofisi ya Ardhi Kanda ya Kaskazini kuhaskikisha inatoa mafunzo kwa watunza kumbukumbu za Majalada ya ardhi kwa halmashauri zote za mkoa mzima wa Tanga ili waweze kutunza kumbukumbu vizuri.