Na Stella Kalinga, Simiyu RS
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, anayeshughulikia masuala ya watu wenye ulemavu, Mhe. Stella Ikupa, amefunga rasmi kambi ya kitaaluma kwa wanafunzi wa kidato cha nne Mkoani Simiyu, ambapo amewapongeza viongozi wa mkoa wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Anthony Mtaka kwa ubunifu huo ambao utawasaidia wanafunzi hao kufanya vizuri katika mitihani yao.

Naibu Waziri Ikupa ameyasema hayo Oktoba 30, 2019 wakati wa kuhitimisha kambi ya kitaaluma ya wanafunzi wa kidato cha nne ambayo imefanyika kwa muda wa siku 60 katika Shule ya sekondari Simiyu na Chuo cha Ualimu Bariadi Mjini Bariadi, kwa lengo la kuwaandaa na mtihani wa Taifa unaotarajia kufanyika kuanzia Novemba 04, 2014.

“Nampongeza Mkuu wa Mkoa kwa ubunifu mkubwa wa kuandaa kambi hizi kwani, naamini wanafunzi mmejifunza mambo mengi na mtafanya vizuri katika mtihani wenu, ningeshauri watu wengine waige jambo hili, niwakumbushe wanafunzi mtakaoanza mtihani wenu Novemba 4, 2019, kumuomba Mungu ili awaongoze kipindi chote cha mitihani,” alisema Ikupa.

Aidha, Ikupa amesema Serikali imeendelea kuboresha sekta ya elimu nchi kwa kuongeza bajeti katika shule, kujenga madarasa, na anaamini kuwa itaendelea kutatua changamoto ya walimu katika mkoa wa Simiyu, na nchini kwa ujumla.

Mkuu wa Mkoa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema uongozi wa Mkoa, walimu, wazazi na wadau wote wa elimu mkoani humo wamefanya uwekezaji mkubwa kwa wanafunzi wote waliokuwa katika kambi za kitaaluma na kupitia kazi nzuri iliyofanywa na walimu anaamini kwamba watafanya vizuri katika mtihani wa Taifa utakaoanza Novemba 4, 2019.

Ameongeza Serikali mkoani Simiyu itaendelea kuwapa motisha walimu, wanafunzi na shule zote zitakazofanya vizuri katika mitihani ya Kitaifa, huku akiahidi kuwalinda walimu wote, ambapo ameahidi kuwa kuanzia Desemba Mosi, 2019 viongozi wa mkoa watawatembelea walimu katika Halmashauri zote na kuzungumza nao.

Mkurugenzi wa Idara ya Habari- MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbas amewaomba wadau kuendelea kuunga mkono kambi hizi ili waweze kutimiza ndoto zao huku akibainisha kuwa kupitia kambi hizo watapatikana viongozi mahiri wa baadaye.

Katibu Mkuu, Chama cha Walimu Tanzania, Deus Seif amesema walimu wana imani na Serikali na wameamua kufanya kazi yao kwa bidii na wanaiomba Serikali kuendelea kushughulikia changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwemo kupandishwa madaraja na mishahara kwa wakati na malipo ya fedha za likizo na malimbikizo ya mishahara.

Naye Afisa Elimu wa Mkoa, Mwl. Ernest Hinju amesema tangu kambi hizi zianze mwaka 2016 zimesaidia kuongeza kiwango cha ufaulu katika matokeo ya darasa la saba, kidato cha nne na kidato cha sita, ambapo kwa kidato cha nne mwaka 2017 ufaulu ulikuwa 70.68% na mwaka 2019, ufaulu umekuwa 86.46%.

Naye Diana Boniphace mwanafunzi kutoka Shule ya sekondari Kidinda amesema, “kupitia kambi hii wanafunzi tumejifunza mambo mengi kupitia kwa walimu mahiri na kiwango cha ufaulu kimeongezeka tofauti na tulivyoingia hivyo tunaahidi kuwa tutafanya vizuri katika mtihani wa Taifa tutakaoanza Novemba 04, 2019.”

Kambi ya Kitaaluma iliyohitimishwa Oktoba 30, 2019 ilihusisha wanafunzi 1512 ambao walikuwa na ufaulu hafifu(daraja sifuri), wanafunzi waliofanya vizuri katika mtihani wa Mkoa(Mock) na wanafunzi kutoka shule zenye wanafunzi chini ya 30 na wamekaa kambini siku 60.
 Baadhi ya wanafunzi wa kidato cha nne Mkoani Simiyu wakiwa katika picha ya pamoja na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, anayeshughulikia masuala ya watu wenye ulemavu, Mhe. Stella Ikupa, mara baada ya kambi ya kitaaluma ya siku 60 kwa wanafunzi hao kuhitimishwa Oktoba 30, 2019 Mjini Bariadi.
 Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, anayeshughulikia masuala ya watu wenye ulemavu, Mhe. Stella Ikupa, akizungumza na walimu pamoja na wanafunzi wa kidato cha nne mkoani Simiyu, wakati wa kufunga kambi ya kitaaluma ya siku 60 Oktoba 30, 2019 Mjini Bariadi.
 Baadhi ya wanafunzi wa Kidato cha nne kutoka shule mbalimbali mkoani Simiyu, wakimsikiliza Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, anayeshughulikia masuala ya watu wenye ulemavu, Mhe. Stella Ikupa, wakati wa kufunga kambi yao ya kitaaluma ya siku 60 Oktoba 30, 2019 Mjini Bariadi.
 Kutoka kulia Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, anayeshughulikia masuala ya watu wenye ulemavu, Mhe. Stella Ikupa,Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka, Katibu Tawala Mkoa, Bw. Jumanne Sagini, Afisa Elimu Mkoa, Ernest Hinju na Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga wakifurahia jambo, wakati wa kufunga kambi ya kitaaluma ya siku 60 kwa wanafunzi wa kidato cha nne Oktoba 30, 2019 Mjini Bariadi.
 Baadhi ya wanafunzi wa kidato cha nne Mkoani Simiyu wakishangilia jambo wakati wa hafla ya kufunga kambi ya kitaaluma ya siku 60 kwa wananfunzi wao ambayo imehitimishwa na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, anayeshughulikia masuala ya watu wenye ulemavu, Mhe. Stella Ikupa, Oktoba 30, 2019 Mjini Bariadi.
 Baadhi ya wanafunzi Kidato cha nne kutoka shule mbalimbali mkoani Simiyu wakicheza na kufurahi na Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Anthony Mtaka mara baada ya kufunga kambi ya kitaaluma ya siku 60 Oktoba 30, 2019 Mjini Bariadi.
 Baadhi ya viongozi wakifuatilia kitu wakati wa kufunga kambi ya kitaaluma ya siku 60 kwa wanafunzi wa kidato cha nne Oktoba 30, 2019 Mjini Bariadi , kutoka kulia walioketi mbele, Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt Hassan Abbas, Katibu wa CWT Taifa, Mwl. Deus Seif na Mbunge la Afrika Mashariki, Mhe. Happyness Lugiko ,
 Baadhi ya walimu mahiri waliofundisha kambi ya kitaaluma ya kidato cha nne wakishangilia jambo wakati wa hafla ya kufunga kambi ya kitaaluma ya siku 60 kwa wanafunzi wao ambayo imehitimishwa na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, anayeshughulikia masuala ya watu wenye ulemavu, Mhe. Stella Ikupa, Oktoba 30, 2019 Mjini Bariadi.