Mwanamuziki maarufu wa Rwanda Meddy ametiwa nguvuni baada ya kukamatwa akendesha gari huku akiwa ni mlevi , imesema polisi mjini Kigali.

" Alikamatwa alipokuwa akiendesha gari kwa kasi kupita kiasi huku akiwa amelewa, atafungwa kwa siku tano na kupigwa faini ya ya Franga za Rwanda 150,000 sawa na $150," msemaji wa polisi mjini Kigali Goretti Umutesi, ameiambia BBC.


Meddy ambaye jina lake halisi ni Ngabo Medard ni msanii wa muziki wa R&B, mnyarwanda anayeishi nchini Marekani aliiambia BBC mwezi Agosti kwamba alikuwa anapanga kufanya tamasha nchini Rwanda na mataifa mengine ya Afrika.

Katika miezi ya hivi karibuni polisi ya Rwanda imeimarisha msako dhidi ya watu wanaoendesha magari wakiwa wamekunywa pombe ili kukabiliana na ajali za barabarani.


”Mimi ni Mrundi na Mnyarwanda...” Mwanamuziki Meddy akiri
Wiki mbili za mwezi Septemba watu 191 walikamatwa na kupigwa faini kwa kunywa pombe na kuendesha magari, na mwezi Agosti zaidi ya watu 700 walishtakiwa kwa kosa hilo.

Licha ya kulipa faini ya dola $150, baadhi ya washukiwa wamekuwa wakifungwa kwa siku kadhaa, hatua ambayo imekuwa ikikosolewa kuwa ni kinyume cha sheria.

Wakosoaji pia wanasema badhi ya polisi hawana kipimo cha kupima kiwango cha pombe alichokunywa mtu na kuthibitisha kwamba madereva wamekiuka viwango vya pombe kinachopaswa kuwa katika damu.