Mahakama  ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Uwekezaji (ICSID), imeiamuru Tanzania kulipa Dola za Marekani milioni 185 pamoja na riba kwa madai ya uharibifu ilioufanya kwenye Benki ya Standard Chartered (Hong Kong) kuhusu mzozo wa akaunti ya IPTL Escrow.

Hata hivyo, Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk. Hassan Abbas jana kupitia ukurasa wake wa Twitter, alitoa ufafanuzi wa hukumu hiyo na kusema kuwa deni hilo siyo la serikali bali ni la Kampuni ya Kufua Umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL).

Katika maelezo yake Dk. Abbas alisema kuwa serikali itahakikisha wanasimamia utawala wa sheria ili IPTL ilipe deni lao.

"Nimekuwa nikiulizwa kuhusu kesi zilizoamuliwa za Benki ya Standard Chartered (Hong Kong) dhidi ya Tanesco na sasa serikali. Msingi wa kesi zote mdaiwa si serikali wala Tanesco, ni deni la Benki dhidi ya IPTL walilorithi miaka mingi kutoka wakopeshaji wa Malaysia."

"Kwa muktadha huo na kisheria serikali na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) ziliunganishwa tu kama kanuni za kisheria zinavyomruhusu mdai kuwaunganisha wahusika wengine kwenye kesi ili kuhakikisha au kupata uhakika kuwa analipwa madai yake," alifafanua.

Dk. Abbas aliwatoa wasiwasi Watanzania kuwa serikali haidaiwi na haijawahi kukopa Standard Charterd ya Hong Kong.

"Ila kama Baraza la Usuluhishi lilivyoamua, tutahakikisha tunasimamia utawala wa sheria kwa kuona IPTL wanalipa deni lao," alisema.

Hukumu ya kesi hiyo ilifanyika Oktoba 11, mwaka huu na jopo lililosikiliza shauri hilo liliundwa na David Unterhalter kutoka nchini Afrika Kusini, aliyeteuliwa na mlalamikaji na Kamal Hossain kutoka nchini Bangladeshi aliyeteuliwa na mlalamikiwa.

Julai 11, mwaka 2016 Unterhalter aliteuliwa baada ya kujiuzulu kwa Stanley Burnton kutoka Uingereza.Wawakilishi wa mlalamikaji walikuwa ni Herbert Freehills kutoka Uingereza na wa mlalamikiwa ni kampuni ya uwakili ya Crax Low Partners na Rweyongeza and Company Advocates za jijini Dar es Salaam.

Mwaka jana pia, mahakama hiyo ya ICSID iliikataa rufani ya Tanesco ya kupinga hukumu ya kuilipa Benki ya Standard Chartered Dola za Marekani milioni 148.4 sawa na Sh. bilioni 336.

Katika kesi hiyo, Rais wa ICSID, Claus von Wobeser alitupilia mbali hoja za Tanesco za kuitaka mahakama hiyo kutengua uamuzi wa awali ulioipa ushindi benki hiyo ya Hong Kong, nchini China.

Fedha hizo ni madai ya malipo ya umeme baina ya Tanesco na IPTL iliyopewa zabuni ya kufua umeme wa dharura kuanzia Mei 26, mwaka 1995 huku ikidaiwa na benki hiyo.