Na James K. Mwanamyoto, Songea 
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst), Mhe. George H. Mkuchika (Mb) amewapongeza Watumishi wa Umma wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma kwa kutoa msaada wa fedha, sabuni za kufulia na mafuta ya kula kwa watoto yatima wa kituo cha Swako kilichopo Songea mjini kwani wameonyesha taswira nzuri ya utumishi wa umma kwa wananchi ambao ndio walengwa wakuu wa huduma zitolewazo na taasisi za Serikali.

Mhe. Mkuchika ametoa pongezi hizo alipokutana na Watumishi wa Umma kwenye ziara yake ya kikazi yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma, ikiwa ni pamoja na kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini mkoani humo.

Akikabidhi msaada huo kwa niaba ya watumishi hao, Mhe. Mkuchika amewashukuru watumishi waliochanga fedha hizo na kutoa mahitaji mengine ambayo yamekuwa ni faraja kwa watoto hao.
“Msaada mlioutoa utakuwa ni chachu ya kujenga ustawi wa watoto hao ili hapo baadae waweze kuwa na mchango katika maendeleo ya taifa, na ndio maana mmemuona mlezi wa kituo hicho amefurahi sana baada ya kupokea msaada wenu”, Mhe. Mkuchika amesisitiza.

Msaada walioutoa watumishi hao ni mwendelezo wa utekelezaji wa maelekezo ya Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro ya kuzitaka  taasisi za umma nchini kuadhimisha Wiki ya Utumishi wa umma mwaka huu kwa kushiriki masuala ya kijamii ili kujenga uhusiano mzuri na wananchi. 

Aidha, Mhe. Mkuchika amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Mhe. Christina Mndeme na Katibu Tawala wa Mkoa huo, Prof. Riziki Shemdoe kwa kuratibu vema utekelezaji wa maelekezo ya ofisi yake katika kuadhimisha Wiki ya Utumishi wa Umma mwaka huu kwani pamoja na kutekeleza maagizo mengine wakati wa wiki hiyo ambayo huadhimishwa tarehe 16 hadi 23 Juni kila mwaka lakini waliona pia ni vema wakawasilisha msaada kwa watoto yatima .

Awali, Katibu Tawala Mkoa wa Ruvuma, Prof. Riziki Shemdoe alimueleza Mhe. Mkuchika namna watumishi wa Sekrekarieti ya Mkoa wa Ruvuma walivyojitoa kuchanga fedha hizo na kuhakikisha wanashiriki kikamilifu shughuli za ustawi wa kijamii ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma nchini.

Mhe. Mkuchika anaendelea na ziara ya kikazi mkoani Ruvuma yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma, ikiwa ni pamoja na kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini mkoani humo.
 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst), Mhe. George H. Mkuchika (Mb) akifafanua masuala ya kiutumishi kwa watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Ruvuma na Halmashauri ya Wilaya ya Songea (hawapo pichani) wakati wa kikao kazi chake kilichofanyika mjini Songea kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi hao.
 Baadhi ya watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Ruvuma na Halmashauri ya Wilaya ya Songea wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst), Mhe. George H. Mkuchika (Mb) wakati wa kikao kazi chake kilichofanyika mjini Songea kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi hao.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst), Mhe. George H. Mkuchika (Mb) akikabidhi msaada wa fedha taslimu na mahitaji kwa mlezi wa kituo cha Swako cha kulea watoto yatima, Bi. Regina Chinguku kilichopo Songea mkoani Ruvuma kwa niaba ya watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma waliochanga ili kukisaidia kituo hicho.