Mitihani ya Kimataifa ya ujuzi wa lugha ya Kiswahili itaanza kutolewa na Chuo  Kikuu cha Dar es salaam (UDSM), ikiwa na lengo la ukuzaji wa lugha fasaha ya kiswahili kuanzia mwakani 2020.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo ameyasema hayo Jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hatua za ukuzaji wa lugha ya Kiswahili.

Amesema jitihada zimewekwa ili kufanikisha zoezi hilo kwa kuikuza na kuieneza Lugha ya Kiswahili ulimwenguni kote kwa kuhakikisha inakuwa ni miongoni mwa lugha 10 zenye wazungumzaji wengi Duniani.

“Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alifanya jitihada za kuiendeleza na kuieneza Lugha ya Kiswahili pamoja na kusimamia ubora wake ndani na nje ya nchi hatua hii pia imefanywa na viongozi waliofuata sasa ni lazima tufikie lengo,” amesema Dkt Akwilapo.

Ameongeza kuwa mitihani hiyo itakuwa ikifanyika mara sita kwa mwaka ikiambatana na kipindi cha masomo ya Kiswahili kwa kila ngazi na itafanyika kwa njia za kielektroniki katika vyuo na vituo mbalimbali vya Kiswahili duniani walivyofanya navyo makubaliano.

Dkt. Akwilapo amebainisha kuwa  Chuo hicho (UDSM), kitakuwa ni chuo kikuu cha kwanza duniani kutunga mitihani hiyo huku kikisimamia utahini na usahihishaji wake sambamba na kutoa cheti cha Kimataifa.

“Cheti hiki kitakuwa kinaonesha kiwango cha ujuzi wa mtahiniwa maana ili kujua mhitimu amekuwa na ujuzi wa lugha kwa kiasi gani ni lazima kujipima kwa lengo la kupata ukweli wa jinsi gani tunasogea katika ukuzaji lugha ya Kiswahili,” amefafanua Dkt. Akwilapo.

Aidha Akwilapo amebainisha kuwa chuo hicho pia kimechukua jukumu la kuanzisha mitihani ya Kimataifa ya ujuzi wa lugha ya Kiswahili Sanifu kwa lengo la kupata nguvu kimataifa na kwamba hutungiwa mitihani ili wanaojifunza wafanyiwe tathmini na kupata vyeti.

“Tayari UDSM imejiandaa kuhakikisha mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano iko madhubuti kuwezesha mitihani hii kufanyika kwa ufanisi na kwa viwango vya kimataifa maana kuna watu ambao watafanya mitihani hii wakiwa katika nchi zao,” amebainisha Dkt. Akwilapo.

Awali Mkurugenzi wa Taasisi ya Taaluma za Kiswahili Prof. Aldin Kai Mutembei amesema mitihani hiyo itakuwa ikiitwa jina la mkuki na kwamba tayari kuna makubaliano baina ya walimu wa Kiswahili wa UDSM na wale wanaofundisha Kiswahili katika vyuo vya nje.

Zimbabwe: Tembo 55 wafa kwa kukosa maji ya kunywa
“Kuna wanafunzi wanasoma Kiswahili nje na wanatamani kuja kwenye nchi zinazozungumza lugha hiyo lakini wangependa wawe na utambulisho kuwa wanajua Kiswahili na ndio maana tukaona ipo haja ya kufanya mitihani ya aina hii na tunatarajia kuwa mabalozi wazuri kwa kuiwakilisha Serikali katika ukuzaji wa lugha ya Kiswahili,” amesema Prof. Mutembei