Kibano watoto wanaofanya biashara stendi za mabasi
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka Wakuu wa Wilaya za Itigi na Ikungi na Wakurugenzi wao wafanye misako kwenye stendi za mabasi ili kuwabaini watoto wasiokwenda shule.

Ametoa agizo hilo kwa nyakati tofauti jana, wakati akihutubia mamia ya wananchi waliojitokeza kumsikiliza kwenye mikutano ya hadhara aliyoifanya kwenye wilaya hizo.

Alisema Serikali ya awamu ya tano imeondoa michango kwenye sekta ya elimu na kwa maana hiyo watoto wenye umri wa kwenda shule wanapaswa wawe shuleni.

“Michango ya hovyohovyo haipo, vinginevyo, fedha ambazo wazazi mmeokoa, peleka kwa mtoto, mnunulie sare, kiatu kizuri, begi la shule na madaftari. Ale vizuri asubuhi na aende shule,” amesisitiza Waziri Mkuu.

“Hatutarajii kuona vijana wadogo wanauza biashara kwenye vituo vya mabasi. Mkurugenzi chukua OCD siku moja, nenda kwenye miji yenu midogo, saka watoto wote wanaofanya biashara stendi.”

“Watambue wazazi wao, halafu kamata wazazi hao wajieleze ni kwa nini wanawaacha watoto wao waende kuhangaika stendi badala ya kwenda shule, tunataka kila mtoto wa Kitanzania aende shule,” ameagiza Waziri Mkuu.

Aidha amesema Serikali imetoa maelekezo kwamba kila kijiji kinapaswa kiwe na shule ya msingi na kila shule lazima iwe na darasa la awali ili watoto wenye umri wa miaka minne hadi mitano waanze shule mara moja.