Vyama vya siasa vinavyokusudia kusimamisha wagombea wake kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 24, 2019 vimetakiwa kuzingatia kanuni zilizowekwa ili kuhakikisha unafanyika bila ya kasoro.

Wito huo umetolewa na Waziri wa nchi ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jafo Jijini Dodoma Octoba 28, 2019 na kuonya wagombea kutofanya shamrashamra wakati wa kuchukua fomu.

“Wale wote wenye nia ya kuchukua fomu za ugombea suala la mbwembwe au shamrashamra haliruhusiwi kama sehemu ya kampeni tunahitaji uchaguzi huu uwe wenye kuzingatia kanuni na taratibu zilizowekwa ili ukamilike bila dosari,” ameongeza Jafo.

Waziri Jafo ambaye alikuwa akizungumza na waandishi wa Habari amefafanua kuwa zoezi la uchukuaji fomu za ugombea kwenye uchaguzi huo linaanza leo Oktoba 29, 2019 na linatarajia kukamilika Novemba 4, 2019.

Aidha ametoa wito kwa wasimamizi wa uchaguzi kuhakikisha hawaingilii zoezi hilo huku akivitaka vyama vya siasa kuzingatia misingi ya kidemokrasia ikiwemo kuwadhamini wagombea wao.

“Vyama vijitahidi kuheshimu misingi ya kidemokrasia na viwadhamini wagombea wao lakini pia nawaonya wenyeviti wa mitaa na vitongoji ambao muda wao umekwisha tangu octoba 22 hawatakiwi kufanya jambo lolote kinyume cha sheria,” amesisitiza Jafo.

Wakati zoezi la uchukuaji fomu za kugombea uongozi katika uchaguzi wa serikali za mitaa likiwa tayari limetangazwa rasmi uchaguzi huo unatarajia kufanyika nchini kote Novemba 24, 2019.