Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto anayeshughulikia Maendeleo ya Jamii amewataka Maafisa Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii nchini kuchapa kazi kwakua ni watu muhimu sana katika maendeleo ya taifa.

Katibu Mkuu Jingu ameyasema hayo mkoani Mtwara wakati akizungumza na Maafisa Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii kutoka Halamshauri na Wilaya za Mikoa ya Lindi na Mtwara.

Ameongeza kuwa fani za Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii ni muhimu katika kuisaidia Serikali katika jitihada za kuwaletea wananchi maendeleo nchini hivyo Maafisa hao wanatakiwa kufanya kazi kwa weledi ili kulifanikisha hilo.

Dkt. Jingu amesema kuwa lengo la kukutana na Maafisa hao ni kuzungumza na kujadiliana kwa undani namna ya kuzifanya fani za maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii ziweze kusaidia maendeleo ya nchi.

Dkt. Jingu amesema kuwa Wizara inaratibu uwepo wa mazingira mazuri ya kuwezesha Maafisa Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii ili kuwawezesha Maafisa hao kutekeleza majukumu yao hasa katika ngazi ya Kata na mitaa.

Aidha Dkt. Jingu amewataka maafisa hao kuifanya jamii kuona umuhimu uwepo wa Maafisa Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii katika maeneo yao kwa kuwezesha kuamsha ari ya wananchi katika kujiletea maendeleo wenyewe.

Naye Kamishana wa Ustawi wa Jamii nchini Dkt. Naftali Ng’óndi amesema kuwa Wizara inajipanga kuwa na mkutano wa mwaka wa kuwakutanisha Maafisa Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii ili kujadiliana changamoto zinazowakabili na kuzipatia ufumbuzi ili kuleta ufanisi wa utekelezaji wa majukumu yao.

Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara Bw. Emmauel Mwakajila amesema amipongeza Wizara kwa kuja kuwasikiliza katika maeneo yao ya kazi na kujua changamoto zinazowakabili ili kuwezesha kupatikana kwa utatuzi wake.

Naye Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Newala Bi. Christina Kambuga amezitaja changamoto za vifaa, watumishi kuwa ni tatizo kubwa katika Idara ya Ustawi wa Jamii katika Halmashauri hasa uhaba wa Maafisa Maendeleo ya Jamii katika Kata.

Aidha Afisa Ustawi wa Jamii kutoka Sekretarieti ya Mkoa wa Lindi Bi. Stellah Kihombo amesema kuwa kumekuwa na changamoto ya utekelezaji wa majukumu yao ikiwa ni kutokuwa na uelewa wa pamoja kati ya Maafisa Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa jamii katika maeneo mengi nchini.

Katibu Mkuu amekutana na Maafisa Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii kutoka Halmashauri za Wilaya za mikoa ya Lindi na Mtwara kujadiliana na kujua changamoto katika utekelzaji wa majukumu yao.
 Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto anayeshughulikia Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu akizungumza na maafisa Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii kutoka Halmshauri za Wilaya za mikoa ya Lindi na Mtwara kilichofanyika katika ukumbi wa Benki ya Tanzania mkoani Mtwara.
 Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Newala Bi. Christina Kambuga akieleza changamoto za utendaji kazi kwa kada ya Maendeleo ya Jamii katika Halmashauri wakati wa kikao kati ya Katibu Mkuu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto anayeshughulikia Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu na maafisa Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii kutoka Halmshauri za Wilaya za mikoa ya Lindi na Mtwara.
 Afisa Ustawi wa Jamii kutoka Sekretarieti ya Mkoa wa Lindi Bi. Stellah Kihombo akieleza changamoto za utendaji kazi kwa kada ya Ustawi wa Jamii katika Halmashauri wakati wa kikao kati ya Katibu Mkuu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto anayeshughulikia Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu na maafisa Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii kutoka Halmshauri za Wiaya za mikoa ya Lindi na Mtwara.
  Maafisa Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii kutoka Halmashauri za Wilaya ya Lindi na Mtwara wakimsikiliza Katibu Mkuu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto anayeshughulikia Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu katika kikao kilichofanyika katika Ukumbi wa Benki ya Tanzania Mtwara.
Katibu Mkuu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto anayeshughulikia Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu akiwa katika picha ya pamoja na Maafisa Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii kutoka Halmashauri za Wilaya ya Lindi na Mtwara mara baada ya kikao kilichofanyika katika Ukumbi wa Benki ya Tanzania Mtwara.