Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt. Anna Peter Makakala Jumatatu Oktoba 7, 2019 amewataka Maafisa Uhamiaji Mikoa yote nchini kuimarisha Mapambano dhidi ya Wahamiaji haramu.

Akizungumza na Watumishi wa Uhamiaji Mkoa wa Rukwa (mjini Sumbawanga), Dkt. Makakala amesema kuwa nchi yetu inaelekea kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na baadae Uchaguzi Mkuu. Hivyo Maafisa Uhamiaji Mikoa yote nchini wametakiwa kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo kwa kutoa Elimu kwa umma pamoja na kuhakikisha kuwa Wahamiaji haramu hawashiriki zoezi hilo.

Kwa ushirikiano na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Idara ya Uhamiaji inatarajia kutoa Elimu ya Uraia kwa kuanzia na Mikoa ya Kagera, Kigoma, Rukwa, Katavi na Geita. Maafisa Uhamiaji wote nchini wametakiwa kuandaa vipindi maalum vyenye lengo la kuwajengea uwezo na uzalendo wananchi hususan katika masuala ya Uraia.
“Kila Mwananchi anao wajibu wa kulinda usalama wa nchi yetu kwa kutoa taarifa za Wahamiaji haramu. Kumhifadhi au kumsaidia Mhamiaji haramu kupata kitambulisho cha mpiga kura na kushiriki zoezi la kupiga kura kwa ama kuchagua au kuchaguliwa ni kukosa uzalendo kwa nchi yetu” amesisitiza Dkt. Makakala.

“Taifa lolote Duniani liwe kubwa au dogo haliwezi kukamilika bila ya raia wake kwani raia hao ndio wenye nchi na wanaotakiwa kunufaika na haki zitolewazo na serikali kwa raia wake kwa mujibu wa katiba ya nchi ikiwa ni pamoja na haki ya kuchagua au kuchaguliwa katika nafasi za uongozi Kwa upande mwingine ni raia hao ndio wenye wajibu wa kulinda nchi yao” aliongeza Dkt. Makakala.

Awali akitoa taarifa ya Utendaji kazi katika Mkoa wa Rukwa, Afisa Uhamiaji Mkoa wa Rukwa, Naibu Kamishna wa Uhamiaji Elizeus Mshongi ameeleza kuwa mkoa wa Rukwa unapokea idadi kubwa ya wahamiaji haramu, wengi wao wanatoka katika Mataifa ya Zambia, D.R Congo na Burundi.
Kwa kipindi cha cha kuanzia Januari hadi Agosti, 2019; jumla ya wahamiaji haramu 128 wamekamatwa na kuchukuliwa hatua mbalimbali ikiwamo kushitakiwa na kuondoshwa nchini.

Naibu Kamishna Mshongi ameongeza kuwa Mkoa unaendesha zoezi la kuwatambua na kuwaorodhesha Wahamiaji walowezi. Kupitia Zoezi hilo jumla ya Walowezi 5,743 wametambuliwa na kuorodheshwa.

Aidha, Idara ya Uhamiaji inatoa wito kwa Wahamiaji walowezi wote wanaoishi nchini kujitokeza na kujiorodhesha, watakaoshindwa kufanya hivyo hatua za kisheria zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani na kuondoshwa nchini.