SERIKALI jana Alhamisi, Oktoba 17, 2019, iliagiza watoto wa aliyekuwa mfanyabiashara mkubwa nchini, bilionea Erasto Msuya,  warudishwe kwenye makazi ya baba na mama yao ambayo yalikuwa yamefungwa.



Agizo hilo la awali limetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Jerry Muro,  baada ya kukutana na wazazi wa hayati Msuya, watoto wake na baadhi ya wanafamilia upande wa mke wa Msuya ambaye yupo Gereza la Segerea jijini Dar es Salaam akikabiliwa na kesi ya mauaji ya wifi yake, Anette Msuya,  ambaye alikuwa dada wa mumewe.



Wakizungumza baada ya uamuzi huo, mtoto wa bilionea huyo, Kelvin Msuya na babu yake, Elisaria Msuya walikubaliana na uamuzi huo wa awali.



Kijana Kelvin (22) ambaye aliripotiwa na Global TV Online akimwomba Rais Magufuli awasaidie kupata mali za baba yao, anasema anataka yeye na wadogo zake wapewe haki ya kusimamia mali za baba na mama yao na si mtu mwingine.

Anasema familia ya baba yao inataka kuwanyan’ganya mali kwani baada ya mama yao kukamatwa wamefungua kesi upya za kudai usimamizi wa mirathi ingawa tayari mama yao aliteuliwa wa lengo la wao wachukuwe mali.



“Mwanzo babu na shangazi Esther walifungua kesi ikafutwa, Ndeshukuro Sikawa na babu wakafungua ikafutwa sasa amefungua tena bibi peke yake,” amesema.



Anasema ndugu hao walimfungulia kesi na kutaka kumuunganisha na mama yake lakini alisaidiwa na ndugu wa mama yake na maafisa wa juu wa polisi.



Hata hivyo,  baba wa billionea huyo, anasema walifunga nyumba za billionea huyo kutokana na kuzuia upotevu wa mali hasa baada ya kuanza kuibiwa.



Alisisitiza baadhi ya mali za billionea huyo, yeye na mkewe, walikuwa na hisa ukiwemo mgodi wa Tanzanite ambao alidai ni mali yake, hoteli ya SG na mashamba.



Msuya aliuawa kwa kupigwa risasi mwaka Agosti 7, 2013 na ameacha nyumba za kifahari zaidi ya tano, magari, hoteli mbili za kitalii, viwanja na mgodi wa Tanzanite.