Msanii wa muziki wa Bongo Fleva, Harmonize amejikuta akiingia kwenye lawama na waandishi wa habari nchini Kenya baada ya kuwachelewesha na kukataa kujibu maswali kwenye mkutano wake na wanahabari.



Imeelezwa kuwa mkutano huo na waandishi wa habari ulipangwa ufanyike saa 5:00 asubuhi lakini ukabadilishwa ratiba mara mbili kuwa ungefanyika saa 9:00 alasiri na baadae ukatajwa tena kufanyika saa 1:00 usiku katika jengo la Kenrail Towers.



Licha kuchelewa kuanza kwa mkutano huo, Waandishi wa Habari nchini humo wamesema kuwa aliongea kwa dakika zisizopungua 3 na kisha kukataa kujibu maswali yanayohusu lebo yake ya zamani ya WCB.

Waandishi wamesema awali kabla ya mkutano huo, Waliambiwa na waandaji wa tukio hilo kuwa kutakuwa na mahojiano ya mmoja mmoja baada ya kumalizika kwa mkutano huo lakini haikufanyika hivyo.

Mwanamuziki huyo alifika katika ukumbi huo wa mkutano na wanahabari akiwa ameongozana na walinzi wake wanne na baadhi ya waandaaji wa mkutano huo.



Bongo5 imeongea pia na moja ya mwandishi aliyekuwepo kwenye tukio hilo,  Bloga Ommy Dallah amesema kuwa Harmonize aliingia na kuongea muda mfupi kisha kuondoka na kuna baadhi ya waandishi walijipanga kufanya nae mahojiano.

“Tulikosa hadi picha, Aliingia na kutoka kwa msanii mkubwa kufanya vile ni mbaya. Kwani tulibaki kama mashabiki wake tu hatukufanya kazi,” amesema Ommy Dalla.

Hata hivyo, Tumejitahidi kutafuta upande wa Harmonize kuzungumzia tukio hilo lakini jitihada zimegongwa mwamba.

Baada ya tukio hilo, Imeelezwa kuwa Harmonize alienda kwenye kipindi cha 10 over 10 kutambulisha wimbo wake wa UNO.

Waandishi wengi wamesema kuwa walistahili kuheshimiwa kama alivyowaheshimu wanahabari wa Tanzania wakati akitambulisha wimbo huo.

Kwa mujibu wa Gazeti la The Star, Harmonize alisafiri kwenda nchini Uganda kwa ajili ya kutambulisha wimbo wake mpya wa UNO.

Chanzo: Gazeti la The Star