Rapa Chid Benz amejibu madai ya watu wanaomsema kwenye mitandao ya kijamii kwamba anaropoka kupita kiasi kwenye baadhi ya mahojiano anayofanya pamoja na kutokuwa sawa kiakili.

Chid Benz amesema hayo alipodakwa na EATV & EA Radio Digital, kwenye sherehe za miaka 12 ya Samaki Samaki Mlimani City, ambapo amesema yeye haropoki na hawezi kumzuia mtu anayemuandika vibaya kwenye mitandao ya kijamii.

"Sijawahi kuropoka, hakuna anayehisi au nani aliyewahi kukuambia maneno hayo nitajie nimfuate. Hakuna aliyeniambia kama nalopoka na kuna muda huwa nasoma maoni ya watu kwenye mitandao ya kijamii, hakuna ubaya kwa mtu akiongea mitandaoni", ameeleza Chid Benz.

Aidha Chid ameongeza kuwa, "siku zinakwenda na mitandao inasogea na kila mtu anatumia bundle lake, huwezi ukamkasirikia mtu ambaye yupo Tabata au Mikocheni akiwa na simu yake anamuandika Chid Benz mitandaoni, ambaye yupo kwenye simu na yule sio mimi maana sitoshi kwenye simu naingiaje humu", ameongeza.

Pia amewataka watu kutofautisha sana kati ya Chid Benz ambaye wanamuona kwenye simu zao kupitia mitandao ya kijamii na jinsi alivyo yeye kwa sababu kwenye simu anajulikana kama Chid Benz lakini kiuhalisia anajijua kama Rashid Abdallah Makwilo.